IDADI YA WALIOKUFA MAAFA YA MAFURIKO KAHAMA YAFIKIA 47
IDADI ya watu waliofariki kutokana na mvua kubwa ya mawe, iliyopewa
jina la tonado, sasa imefikia watu 47 baada ya majeruhi mwingine
aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama kufariki dunia
juzi.
Taarifa ya ongezeko la vifo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Dk Ally Rufunga alipokuwa akipokea misaada ya waathirika wa
maafa hayo kutoka kwa watu mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa
Chadema, Freeman Mbowe na mwakilishi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa.
Pia Rufunga alipokea misaada kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa
Machibya ambaye alikabidhi vyakula na mafuta ya kula aina ya mawese lita
400, sabuni za kufulia katoni 32, chumvi kilo 357, dagaa gunia 12,
mchele kilo 200 na maharage kilo 815.
Vitu hivyo vilitolewa na wakazi wa mkoa wa Kigoma wa ajili ya kuwasaidia waathirika hao.
Akikabidhi msaada kwa niaba ya familia ya Lowassa, Mwenyekiti wa CCM
mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alisema baada ya kutokea kwa maafa hayo,
wanafamilia hao waliguswa na tukio hilo na hivyo kuona umuhimu wa
kuwasaidia wahanga wa maafa hayo kwa kutoa Sh milioni 5.
Mbowe kwa niaba ya chama wache alitoa Sh milioni 10 na aliwataka
Watanzania kutochanganya mambo ya kisiasa, yanapotokea majanga ya
kitaifa, akitoa mfano wa tukio la Mwakata.
Akipokea misaada hiyo, Dk Rufunga aliwapongeza Lowassa na Mbowe kwa
jinsi walivyoguswa na tukio hilo na kwamba misaada waliyoitoa itapunguza
makali ya matatizo yaliyojitokeza baada ya mvua kubwa, iliyoleta
madhara kwa wakazi wa Mwakata.
“Kwa niaba ya mkoa wa Shinyanga tunawashukuru wote walioonesha moyo
wa upendo wa kuwasaidia waathirika hao, tunakushukuru sana, mpaka sasa
tunaendelea kupokea misaada mbalimbali kwa ajili ya kaya 649
zilizoathiriwa na mvua hiyo,” alieleza Rufunga.