Wananchi Chunya walala chini wakiomba waziri mkuu kuigawa wilaya yao
Waziri
mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameahidi kuigawa wilaya ya Chunya ili
kupata wilaya mbili kabla ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika
mwezi Oktoba mwaka huu.
Uamuzi wa waziri mkuu kuigawa wilaya ya Chunya haraka unatokana na
maombi ya wananchi wa jimbo la Songwe hususan katika kijiji cha Buyuni
ambao wameamua kulala chini kwenye mavumbi, huku mbunge wa jimbo la
Songwe, Mheshimiwa Philip Mulugo akipiga magoti chini na kumwomba waziri
mkuu kuigawa wilaya hiyo kwa madai kuwa ina maeneo makubwa kijiografia
hali ambayo inakwamisha maendeleo ya wananchi.
Mkuu
wa mkoa wa Mbeya akamweleza waziri mkuu kuwa ukubwa wa wilaya
ya Chunya ni asilimia 46 ya ardhi yote ya mkoa wa Mbeya hivyo maombi ya
wananchi hao yana hoja ya msingi, huku wa wilaya ya Chunya Deodatus
Kinawiro akielezea uwezo wa halmashauri ya wialaya ya Chunya kiuchumi
kuwa inajitegemea kwa asilimia 15.
Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda amesema kuwa kikwazo pekee cha
kuigawa wilaya hiyo ni idadi ndogo ya watu, lakini kutokana na hali
ambayo ameiona analazimika kuigawa wilaya hiyo haraka, jambo ambalo
ameahidi kulifanya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.