MWANAFUNZI WA SEKONDARI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUMUUA ASKARI WA JWTZ KWENYE MAPIGANO YA AMBONI TANGA
WAKAZI 10 wa jijini hapa, akiwemo mwanafunzi wa sekondari
wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa
matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya polisi silaha pamoja na
kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti
Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari (19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa tisa wameelezwa kuwa ni wafanyabiashara, nao ni Mbega Seif
(25) maarufu ‘Abuu Rajab’ mkazi wa Kiomoni, Amboni, Ayubu Ramadhani
(27) maarufu ‘Chiti’ ambaye ni fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni,
Hassani Mbogo (20) maarufu ‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora, Mohamed
Ramadhani (19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25)
maarufu ‘Kizota au Kisaka’ mkazi Magaoni.
Washtakiwa wengine ni Saidi Omari (26) mkazi wa Magaoni Tairi Tatu,
Nurdin Mbogo (27) Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa Donge pamoja
na Omari Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa Dunia Hoteli
Makorora.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa
Serikali, George Barasa akisaidiana na MariaClara Mtengule, walidai
kuwa kosa la kwanza hadi la tatu linawahusisha washitakiwa namba moja
mpaka nane (1 -8) ambao wanatuhumiwa kushiriki kula njama ya kutenda
kosa kinyume cha sheria.
Barasa alidai kuwa katika maeneo tofauti ya jijini Tanga kati ya
Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu, washitakiwa wote wanane
kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa la unyang’anyi
wa silaha.
Katika kosa la pili, Barasa alidai mahakamani hapo kwamba mnamo
Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali ulipo kati ya barabara ya
Nne na ya Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane waliiba silaha
moja aina ya SMG namba za usajili 14303545 mali ya Polisi na muda mfupi
kabla ya kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu
ili kupata silaha hiyo.
Kosa la tatu la washitakiwa hao ni unyang’anyi wa kutumia silaha, na
washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa katika mgahawa wa Jamali uliopo
kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha nyingine yenye namba
za usajili 14301230 SMG mali ya polisi na kwamba muda mfupi kabla ya
kutenda kosa hilo walimtishia kwa kutumia nguvu kumnyang’anya silaha PC H
Mansoor kinyume na sheria.
Hata hivyo, katika kosa la nne ambalo limemhusisha mshitakiwa namba
tisa Nurdin Mbogo wakili huyo wa Serikali, alidai kuwa Februari 6 mwaka
huu, katika sehemu isiyofahamika jijini Tanga, mshtakiwa huyo akijua
kuwa Hassan Mbogo (Mshitakiwa Na. 4) alitenda kosa Septemba mosi 2014 na
Januari 26 mwaka huu alimsaidia kumwezesha kukwepa kushtakiwa na
kuadhibiwa kinyume na sheria.
Katika hatua nyingine, Wakili wa Serikali Mtengule alisoma shitaka
jingine jipya ambalo liliwahusisha watuhumiwa watatu akiwemo namba 1 na 2
(Mbega Rajabu na Rajabu Bakari) pamoja na mshtakiwa mwingine Omari
Harub Abdallah ‘Ami’ wakidaiwa kwa pamoja kuhusika kumuua askari wa
JWTZ, Sajenti Mohamed Rashid Kajembe mnamo Februari 13 mwaka huu katika
Mapango ya Amboni Jijini Tanga kinyume cha sheria namba 196 na 197 ya
makosa ya adhabu ya mwaka 2002 .
Washtakiwa hao watatu hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Hata hivyo, washitakiwa wote 10 kwa pamoja wamekana makosa yao, na
mahakama imewanyima dhamana washitakiwa tisa kutokana na makosa
waliyotenda kutokuwa na dhamana.
Mshitakiwa namba tisa Nurdin Mbogo alishindwa kutimiza masharti ya
dhamana baada ya kutakiwa kutoa Sh milioni moja na mdhamini mmoja mwenye
mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni moja.
Washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Mnamo Februari 13 mwaka huu katika eneo la Amboni Jijini Tanga
palizuka mapigano baina ya askari polisi wakishirikiana na JWTZ dhidi ya
watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi, waliokuwa wamejificha kwenye mapango
ya Majimoto.
Katika tafrani hiyo, kulisababish kifo cha askari wa JWTZ na majeruhi
watano wakiwemo wanajeshi wawili na Polisi watatu, hali iliyozua hamaki
kwa wakazi wa jijini hapa.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake mwezi uliopita alielezea
matukio hayo kuwa ni ya ujambazi, lakini pia yana mwelekeo wa ugaidi na
akalitaka jeshi la polisi kuwasaka watuhumiwa wote na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria.