UTORO, MIMBA: CHUNYA NI ZAIDI YA KYELA


index
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameendelea kukemea tabia za utoro na mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Chunya baada ya kupewa taarifa kwamba watoto 4,420 walitoroka shule na wengine 201 kupata mimba.



Februari 26, mwaka huu, Waziri Mkuu aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaka na kuwakamata wale wote waliohusika na utoro na ujauzito wanafunzi na kuwafikisha mahakamani mara moja ili liwe fundisho kwa wengine baada ya kuelezwa kwamba wanafunzi 94 walipata ujauzito na wengine 645 kuacha shule kwa sababu ya utoro.



Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumamosi, Februari 28, 2015) kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu alisema haiwezekani kuiacha hali hiyo iendelee huku watoto wa wilaya hiyo wakiharibiwa maisha kwa kukosa masomo.



“Utoro kwenye shule za msingi, taarifa ya wilaya inaonyesha watoto 1,979 waliacha shule kati ya mwaka 2010 na 2014 ambao ni wastani wa watoto 395 kila mwaka na katika suala la mimba, taarifa hiyo inasema watoto 161 waliachishwa shule kwa sababu ya ujauzito,” alisema.



“Haiwezekani kabisa! Hivi akinababa kuamua kutembea na mtoto shule ya msingi ni lipi hasa unalolitaka kwake… unamwachisha shule mtoto kwa lipi hasa, hapana. Nimeshatoa agizo wahusika wakamatwe. Wa zamani tunaweza tusiwapate, lakini hawa wa mwaka jana kwa shule za msingi wako 28, RC na watendaji wako fuatilieni na muwapeleke kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.



Akichanganua takwimu za sekondari, Waziri Mkuu alisema kati ya mwaka 2010 na 2014 wanafunzi 2,251 waliacha shule kwa sababu ya utoro na wengine 40 waliachishwa kwa sababu ya ujauzito.



“Ninawasishi wazazi  na uongozi wa wilaya na mkoa tufanye jitihada kuhakikisha jambo hili linakomeshwa mara moja. Huwezi kununua madaftari an kumlipia ada tu halafu usitake kuona mwanao anamaliza shule. Kila mzazi ana jukumu la kuhakikisha mtoto wake anamaliza shule ili awe na maisha bora hapo baadaye,” alisema Waziri Mkuu.



“Nirudie kuwakumbusha wazazi kwamba mtoto wa mwenzio ni mtoto wako, huwezi kukubali maisha yaharibike hivi hivi. Tuungane pamoja kuhakikisha tunashinda vita hii,” alisisitiza.



Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …