ASKARI POLISI APIGWA CHUPA USONI NA WAENDESHA BODABODA
Askari wa
Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu kama
bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga,
Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya
Temeke.
Akizungumza
kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa kwenye doria kwa kutumia
pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo la Mzinga walimkamata
dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye pikipiki yake.
“Polisi
walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba alikuwa na
makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva wenzake
walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa
kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.
Aliongeza
kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari tunaendelea na
uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze kuwafikisha
mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa kiasi kwamba polisi
walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi za moto hewani.
“Mimi
nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki hapa, walipompiga
yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi hewani.
Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa mashuhuda
aliyeogopa kutajwa jina lake.
Kwa upande
wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana safari ya kwenda Mbagala
na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa risasi na kuamua
kukimbia na kurudi nyumbani.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
Eneo la
Mziga limekuwa na matukio mengi ya kihalifu ambapo mwishoni mwa mwaka
jana kuliibuka kikundi cha kihalifu kilichojiita Black Amerika na
kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.