RADI YAUA MWALIMU NA WANAFUNZI 6 WAKIWA DARASANI
Kamanda wa Polisi Mkoani kigoma, Jafari Mohamed.
Wanafunzi
sita, mwalimu wao, wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa kwa
kupigwa na radi darasani wakati mvua kubwa zilizoambatana na kimbunga
zikinyesha.
Tukio
hilo lilitokea saa 2:30 asubuhi katika Shule ya Msingi Nyakasanda
iliyopo kijiji cha Nyaphenda wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma wakati
mwalimu huyo na wanafunzi hao wakiwa darasani.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kigoma, John Ndunguru, alisema kuwa tukio hilo
lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mvua hizo zikinyesha.
Alisema
mazishi ya mwalimu huyo na wanafunzi hao, yatafanyika leo mchana katika
kijiji hicho chini ya usimamizi wa kamati ya ulinzi ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo Mohamed, alisema majina ya waliokufa yatafahamika leo wakati wa mazishi yao.
Vilevile
alisema wanafunzi wengine 10 na mwalimu wao waliojeruhiwa katika tukio
hilo, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo ya Maweni kwa matibabu.
Wakati
huo huo; watu wanaoshukiwa kuwa majambazi, wamemuua kwa kumpiga kwa
kitu chenye ncha kali Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa
Kigoma (Kiboa), Maneno Jackson.
Kamanda
huyo alisema kuwa mauaji hayo yalitokea usiku wa kuamkia jana baada ya
majambazi hayo kuvamia nyumbani kwa Jackson eneo la Nazareti Manispaa
ya Kigoma Ujiji.
Alisema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.