KESI YA DAWA ZA KULEVYA ZA MABILIONI ZAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATU HAWA HAPA
WATU watano akiwemo raia wa Uingereza wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na
mashitaka ya kukutwa wakisafirisha gramu 2870.781.36 za dawa za kulevya
zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni tano.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa
mashitaka manne mbele ya Mahakimu wawili tofauti. Washitakiwa hao ni
raia wa Uingereza Halid Mahunga, wafanyabiashara Anna Mboya, Fred
William, Kambi Zuberi na Hamis Mtou (32), wakazi wa Dar es Salaam.
Katika mashitaka yanayomkabili Mboya, Wakili wa Serikali Mwandamizi
Evetha Mushi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa kuwa Januari 2,
mwaka 2011 Mboya akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
alikutwa akiingiza nchini gramu 1195.45 dawa za kulevya aina ya cocaine
zenye thamani ya Sh 46,296,200.
Washitakiwa wengine William na Zuberi walifikishwa mbele ya Hakimu
Riwa na kusomewa mashitaka ya kuingiza nchini dawa hizo zenye thamani ya
Sh 5,262,341,700.
Wakili wa Serikali alidai kuwa washitakiwa wanadaiwa Februari 21,
2011 walikutwa Mbezi Jogoo, Wilaya ya Kinondoni wakisafirisha gramu
175.411.36 ya dawa za kulevya aina ya heroine zenye thamani hiyo.
Katika mashitaka yanayomkabili Mtou, Wakili wa Serikali Mwandamizi
Rose Chilongozi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Warialwande Lema kuwa
Novemba 17, 2010 mshitakiwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere alikutwa akisafirisha gramu 811.54 ya dawa za kulevya aina ya
heroine zenye thamani ya Sh 24,346,200.
Aidha katika kesi inayomkabili Mahunga, Mwendesha Mashitaka Thadeo
Mwenemtazi alidai mbele ya Hakimu Lema kuwa Februari 16, 2010 mshitakiwa
alikutwa akisafirisha kete 69 aina ya cocaine gramu 107.40 zenye
thamani ya Sh 50,370,000 kutoka Tanzania kwenda Uingereza.
Katika shitaka la pili Mahunga anadaiwa siku hiyo hiyo alikutwa
akisafirisha gramu 581.38 za dawa hizo aina ya bangi zenye thamani ya Sh
58,138.
Baada ya washitakiwa kusomewa mashitaka yao hawakutakiwa kujibu
chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo
isipokuwa Mahakama Kuu.
Wamerudishwa rumande, kesi zote upelelezi ukiwa umekamilika na watasomewa maelezo ya kesi yao Machi 2 na Machi 3, mwaka huu.