Vifurushi vipya vya mitandao hasa MB 8: TCRA yatoa tamko na maagizo kwa makampuni ya simu
Mamlaka ya mawasiliano nchini, TCRA imetoa tamko kuhusiana na
malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za simu nchini kufuatia
kubadilika kwa vifurushi vya mawasiliano.
Malalamiko hayo yalikuja baada ya baadhi ya mitandao ya simu
kupunguza ukubwa wa data anazopata mtumiaji wa simu anapojiunga na
vifurushi vya muda wa maongezi, sms na data kwa pamoja.
Baadhi ya mitandao imekuwa ikitoa Mega Bytes 8 peke yake ambazo kwa matumizi ya kawaida ni ndogo mno.
“TCRA imechambua mpangilio wa vifurushi – tozo za zamani na mpya na
kugundua kwamba ingawaje baadhi ya watoa huduma wamebadilisha bei, kwa
ujumla bei za muda wa kuzungumza na idadi ya meseji hazikubadilika sana.
"Hata hivyo, kuna upungufu mkubwa kwa idadi ya uniti za data (MBs),”
amesema Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa
John Nkoma kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo
Jumanne.
Kupitia kifungu cha 5 cha Kanuni za tozo (EPOCA Tariff Regulations)
za mwaka 2011, TCRA imeyataka makampuni ya simu kuwasilisha Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania gharama mpya wanazokusudia kutoza wateja wao kabla
hazijaanza kutumika.
Pia imeyataka kupitia upya bei na tozo mpya kwa
kuzingatia mapendekezo hayo na kuwasilisha kwa Mamlaka kama inavyotakiwa
kwa mujibu wa Kanuni za EPOCA za 2011 kuhusu tozo.
“TCRA inawaagiza watoa huduma kuhakikisha kwamba mabadiliko yoyote
yanatekelezwa kidogo kidogo na sio ya ghafla ili kuepuka sintofahamu
katika soko,” imesema.
“TCRA inawaagiza watoa huduma kuwapa wateja wao nafasi ya kuchagua
mpangilio wa vifurushi tofauti kwa huduma wanazohitaji: Kifurushi cha
mazungumzo, Meseji na Intaneti cha siku, siku saba au mwezi ambacho
kinampa mtumiaji uhuru wa kuchagua kiasi ambacho wako tayari kulipia kwa
mazungumzo, meseji na intaneti.”
“TCRA inawashauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua
vifurushi na mpangilio wa tozo ambao unafaa kwa matumizi yao.
"Watumiaji
wanatakiwa kudai taarifa kamili kuhusu huduma wanazozilipia na waelewe
taarifa za watoa huduma kuhusu bei na tozo, ikiwa ni pamoja na vigezo na
masharti ya huduma.
"Mtumiaji asiporidhishwa na huduma anayopata
anatakiwa alalamike – kwanza kwa mtoa huduma wake, na asiporidhika na
ufumbuzi awasilishe malalamiko yake TCRA,” imesisitiza.
“Watumiaji wanashauriwa kuchukua fursa ya soko huria la mawasiliano
nchini kama nafasi ya kulinganisha huduma na bei za watoa huduma na
vifurushi wanavyouza kabla ya kuamua kujiunga na kifurushi chochote au
huduma yoyote.
"Watumiaji wa simu janja zinazowezesha matumizi ya huduma
nyingi, maarufu kama “smart phone”, kuwa makini wakati wa kuzitumia.
Wahakikishe kwamba wanazima maeneo ambayo yanaweza kutumia data hata
kama wakati huo hawatumii vifurushi vya data walivyonunua kwenye
vifurushi.”
Katika hatua nyingine taarifa hiyo imetoa takwimu ya kuongezeka kwa
matumizi ya simu na internet nchini katika kipindi cha miaka 10.
Imesema hadi sasa kuna laini za simu za mkononi zipatazo 31,862,656 ukilinganisha na laini 2,963,737 mwaka 2005.
“Idadi ya simu za mezani ni 151, ukilinganisha na 154, 420 mwaka
2005. Watumiaji wa intaneti wameongezake hadi kufikia 11,000,000
Desemba 2014 kutoka 3,563,732 mwaka 2008.
"Kwa sasa, kuna hamu kubwa ya matumizi ya intaneti na mwelekeo huu utaendelea; hasa kutakapokuwa na ongezeko la mitandao inayowezesha kutoa huduma za intaneti; na kuongezeka kwa mitandao ya jamii,” imesema.
"Kwa sasa, kuna hamu kubwa ya matumizi ya intaneti na mwelekeo huu utaendelea; hasa kutakapokuwa na ongezeko la mitandao inayowezesha kutoa huduma za intaneti; na kuongezeka kwa mitandao ya jamii,” imesema.
“Wateja walionunua laini au ambao wanatumia huduma za simu kwa
kuzungumza imeongezeka kwa asilimia 91 kutoka milioni tatu (3,000,000)
mwaka 2005 hadi milioni 32 ( 32,000,000) mwaka 2014.
"Hii imewezesha
huduma za simu kufikia asilimia 97 ya Watanzania ilipofika Desemba
2014; kutoka asimilia 10 mwaka 2005.
"Kwa upande mwingine, muda wa kuzungumza kwa simu, ukiwa umepimwa kwa dakika zinazotumika, umeongezeka sambamba na ongezeko la idadi ya watumiaji. Umefikia dakika bilioni 41 kutioka dakika milioni 506 mwaka 2005,” imeongeza mamlaka hiyo.
"Kwa upande mwingine, muda wa kuzungumza kwa simu, ukiwa umepimwa kwa dakika zinazotumika, umeongezeka sambamba na ongezeko la idadi ya watumiaji. Umefikia dakika bilioni 41 kutioka dakika milioni 506 mwaka 2005,” imeongeza mamlaka hiyo.
“Matumizi kwa upande wa meseji, yaani SMS na data pia yameongezeka
kwa kiasi kikubwa kutoka SMS zipatazo milioni 5 mwaka 2005 hadi SMS
bilioni 10 mwaka 2014. Watumiaji wa intaneti wanaotumia simu za mkononi
sasa wanafikia milioni 10.”