MLOKOLE: AMTELEKEZA MKEWE KISA KAKATWA MGUU


Kweli Dunia imefikia ukingoni! Mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Josephine Singano mkazi wa Mburahati jijini Dar, amemlalamikia mumewe, Ruwaichi Wilson Manyanga maarufu kama Dk. Manyanga ambaye ni kiongozi wa huduma ya maombezi iitwayo Shalom ya Kanisa la Efatha lililopo chini ya Mchungaji Josephat Mwingira, kwa kumtelekeza.
Mke wa Ruwaichi Wilson, Josephine Singano (anayelia kwa uchungu) aliyetelekezwa na mumewe huyo baada ya kukatwa mguu.
Tukio hilo linadaiwa kuanza mwaka 2013 ambapo Josephine alidai kuwa mumewe alianza kudai kuwa mwanaye wa kwanza aliyemtaja kwa jina la Goodluck kuwa siyo wa kwake na kusema kuwa ameonyeshwa hayo na Roho Mtakatifu.
Josephine alidai kuwa alivumilia maneno hayo ya mumewe kwa muda mrefu ambapo baadaye alianza kuumwa ugonjwa wa kisukari na kutoka kidonda mguuni mwake ambapo hakikupona na kuwa kikubwa kiasi cha kukatwa mguu Februari 14 mwaka 2014.
Katika kipindi chote hicho, Josephine alidai kuwa mumewe ambaye ni daktari wa zahati ijulikanayo kwa jina la Mafalaso, hakuwa akimsaidia kwa kitu chochote jambo lililomfanya kuhama nyumba na kwenda kuishi kwa mama yake mdogo aliyemtaja kwa jina la Neema Juma.
Akizungumza mbele ya Baraza la Usuluhishi, Kata ya Mburahati, Dar Januari 28 mwaka huu, Josephine alidai kuwa amezaa na mumewe watoto watatu lakini anamshangaa kumkataa mtoto wake wa kwanza na kuwakubali wengine wawili huku akidai kutelekezwa baada ya kuwa mlemavu.
“Nimeishi ndani ya ndoa na huyu mwanaume miaka kumi na tisa sasa, nilimshangaa mwenzangu baada ya kuanza kumkataa mwanaye wa kwanza na kutonihudumia mimi kipindi chote nilichokuwa nikiugua. Mbaya zaidi hadi nakatwa mguu hakuwahi kuja hospitali wala kunijulia hali. Kwa kuwa sasa ni mlemavu ndiyo hanitaki kabisa,” alilalama mama huyo huku akimwaga machozi.
Akijibu tuhuma hizo, Dk. Manyanga alisema kuwa Roho Mtakatifu amemuonesha kuwa mtoto anayedaiwa kuwa ni mtoto wake wa kwanza, siyo wake. Alipoulizwa kuhusu kumtelekeza mkewe, alisema kuwa anapenda sana kumsaidia, lakini nafsi yake haimpi msukumo hivyo anachofanya ni kusikiliza Roho Mtakatifi anasema nini kwa kuwa yupo tayari kumsikiliza Mungu kuliko mwanadamu na kuongeza kuwa ugonjwa alionao mkewe ni laana kutoka kwa Mungu kutokana na dhambi alizozifanya.
“Nitamtii Mungu kuliko mwanadamu. Nyinyi hamjui tu huyu mke wangu nilishamkuta mara kibao na mambo ya kishirikina halafu aliwahi kuwa kiongozi wa Efatha kanisani. Alipomwacha Mungu na kwenda hospitali akaishia kukatwa mguu badala ya kudumu kwenye maombezi ambayo Mungu angemponesha, hilo ndiyo jambo linalonifanya niwe mzito hata kumtunza.
“Halafu huyo anayemtaja kuwa ni mwanangu wa kwanza alizaliwa kabla hatujaoana na kila mmoja alikuwa akikaa kwake, hivyo uhakika kama huyo mtoto ni wa kwangu haupo kabisa,” alisema Dk. Manyanga.
Baada ya kuwasikiliza wanandoa hao, wajumbe wa baraza hilo walimtaka Dk. Manyanga na Josephine wafike Februari 3 mwaka huu (leo) katika baraza hilo kwa ajili ya hukumu huku Dk. Manyanga akitakiwa kufika na mtoto wake wa mwisho ambaye ana miaka 3 aliyezaa na Josephine ambaye alidaiwa kumpeleka Moshi bila idhini ya mama yake.
Akizungumza na waandishi wetu, mama mdogo wa Josephine aliyejitambulisha kwa jina la Neema Juma alisema kuwa anamshangaa Dk. Manyanga kwa kuhusisha ukatili wake na Roho Mtakatifu na kuhoji kwa nini asingesema hayo muda wote walioishi katika ndoa yao mpaka aibue suala hilo hivi karibuni wakati mwenzake ni mgonjwa na mlemavu anayeshinda akilia na anahitaji msaada wa mume wake?
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi, Kata ya Mburahati, Khadija Magambo alisema kuwa kama suala hilo halitamalizwa na baraza hilo, basi watalifikisha mahakamani ambapo pande zote mbili zitaamuliwa kisheria.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …