Ajali ya Lori na Pawatila Yaua Watu 7 Manyara
Watu saba wamekufa na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Endagau tarafa ya Endasaki wilayani Hanang’ mkoani Manyara baada ya lori aina ya Fuso kugongana na powatila.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime alisema lori hilo yenye
namba za usajili T 781 AAC likitokea Katesh kuelekea Babati liligongana
na pawatila iliyokuwa imebeba wakulima waliokuwa wakitokea shambani
kuvuna maharage katika kijiji cha Getasam.
Kamanda
Fuime alisema kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa fuso
ambapo lilisababisha kupasuka kwa gurudumu la mbele ndipo lilipoteza
mwelekeo na kuligonga pawatila na kusababisha watu sita kufa papo hapo
na mmoja kupoteza maisha katika Hospitali ya Dareda wakati akipatiwa
matibabu.
Aliwataja
waliokufa ni Uttu (18) Mkazi wa Endasaki, Lazaro Daniel (30) mkazi wa
Kijiji cha Maraa, Agustino Marcel (30) mkazi wa Kijiji cha Maraa,
Inocent (16) Mkazi wa Maraa, Stephano Dahaye (18) Mkazi wa Maraa,
Michael Faustine (25)Mkazi wa Maraa na Elias Leonce (18) naye mkazi wa
Mara aliyefariki dunia akiwa hospitalini.
Aidha
Kamanda Fuime aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Godfrey
Samwel (17), Daniel Yamee (17), Amani Rajabu (19), Isaya Joseph (25),
Hemed Darabe (25), Inocent Ploti na Paulo Anjelus (16) wote wakazi wa
Mara.
Hata
hivyo, Kamanda Fuime alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea na juhudi
za kumtafuta dereva wa Fuso aliyekimbia baada ya kusababisha ajali
hiyo.