Rais Kikwete Apokea Ripoti Ya Oparesheni Tokomeza
Rais Jakaya Kikwete jana alipokea Ripoti ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza katika hafla fupi ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Mara
baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Kikwete aliishukuru Tume kwa kazi
nzuri na kuongeza kuwa amefurahi kuwa suala zima la Operesheni Tokomeza
sasa limefika mwisho wake.
Aidha,
Rais amesema kuwa Serikali itaisoma ripoti hiyo na katika wiki mbili
itatoa maelezo ya jinsi ripoti hiyo itakavyoshughulikiwa.
Rais
Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka kwa Jaji mstaafu Hamisi Msumi,
Mwenyekiti wa Tume ambayo Rais Kikwete aliiteua Mei Mosi, mwaka jana, na
kuitaka ichunguze tuhuma mbali mbali za uvunjifu wa Sheria, Kanuni,
Taratibu na Hadidu za Rejea za Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Aidha,
Rais Kikwete aliipa Tume hiyo jukumu la kupendekeza hatua stahiki za
kisheria za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuhusika na uvunjifu huo.
Vile vile, Rais aliiagiza Tume hiyo ishauri namna bora ya utekelezaji wa
operesheni kama hiyo hapo baadaye.
Rais Kikwete pia aliipa Tume hiyo hadidu za rejea sita ambazo pia ziliainishwa katika Taarifa ya Serikali Nambari 131 ya 2014.
Hadidu
za Rejea hizo ni kama zifuatazo: Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza
ilivyotekelezwa, kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza Operesheni
Tomokeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea
walizopewa, kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza
walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa.
Nyingine
ni kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na
maofisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao
zilikuwa sahihi.
Pia
walitakiwa kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maafisa
wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu za
rejea za Operesheni Tokomeza; na Nyingine ni kupendekeza mambo
yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kupanga na kutekeleza Operesheni
nyingine kama hii, ili kuepuka malalamiko mengine yasitokee.
Jaji
Msumi amemweleza Rais Kikwete kuwa katika kutelekeza majukumu yake,
Tume ilitembelea mikoa 20 na wilaya 38 na kupokea malalamiko mbali mbali
kutoka kwa viongozi wa Serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri wanne
waliojiuzulu kutokana na sakata hilo.
Pia ilipokea malalamiko kutoka kwa watekelezaji wa Operesheni; na walalamikaji na waathirika wa Operesheni.
Jaji
Msumi amemweleza Rais Kikwete kuwa Ripoti ya Tume ina juzuu kumi, juzuu
ya kwanza ikiwa ni Muhtasari wa Taarifa ya Tume, juzuu ya pili ikiwa ni
Taarifa yenyewe ya Tume, Juzuu ya tatu hadi ya tisa ikiwa ni Mwenendo
wa Ushahidi (Proceedings) na Juzuu ya kumi, ikiwa ni vielelezo
vilivyotolewa na mashahidi.