Kardinali Pengo Asali Chini ya Ulinzi Mkali.....FFU Wakiwa Na Mbwa 8 Waliweka Doria Kuimarisha Ulinzi
Katika hali isiyo ya kawaida, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa na mbwa nane, waliweka doria katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika jana.
Ibada
hiyo iliyoanza saa tisa jioni iliongozwa na Paroko wa Kanisa hilo,
Audax Kaasa na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo aliyetarajiwa
kuiendesha kama ratiba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ilivyoeleza,
lakini hakufanya hivyo bali alisali kama muumini wa kawaida.
Gari
ya polisi yenye namba PT 0964 iliegeshwa karibu na lango kuu la
kuingilia kanisani humo, huku mbwa kadhaa wakizunguka katika maeneo
mengine kuangalia usalama na baadaye waliingizwa katika gari hilo.
Haikujulikana
sababu ya ulinzi huo katika kanisa hilo kwa kuwa makanisa mengine
makubwa likiwemo Azania Front hakukuwa na hali hiyo.
Baadhi
ya wadadisi wa mambo wanaihusisha hali hiyo na sakata linaloondelea
kati ya Pengo na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat
Gwajima, aliyemtolea maneno ya kuudhi hali iliyolilazimu Jeshi la Polisi
nchini kuingilia kati.
Akitoa mahubiri, Paroko Kaasa alisema kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha waumini wa Kikristo kumrudia Mungu.
“Mungu
anatutaka turarue mavazi yetu ili tumrudie, kipindi hiki tulipokuwa
tukisikiliza historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo tumesikia
namna alivyodharauliwa.
“Sijui
katika maisha yako kama umewahi kukumbana na dharau aliyokumbana nayo
Bwana Yesu, lakini yote hayo ameyaachia na kusema bwana uwasamehe kwa
kuwa hawajui walitendalo,” alisema Paroko Kaasa.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, alisema kipindi cha Kwaresma ni kipindi ambacho watu
wanafundishwa uvumilivu na msamaha.
“Kipindi
hiki watu tunafundishwa uvumilivu na msamaha, ni vyema kati ya dini na
dini tukajifunza kuvumiliana na tukajifunza kutokutukanana.
“Kipindi
hiki ni mwafaka kukumbushana uvumilivu kwa sababu dini zote duniani
ndiyo nguzo ya amani na uadilifu, mafunzo yote yanayohusu amani na
uadilifu ndiyo nguzo maalumu katika kudumisha amani ya nchi,” alisema Membe.
Katika
hatua nyingine, alisema atatoa ufafanuzi leo kuhusiana na taarifa za
kuwepo kwa vifo vya wanafunzi wa Watanzania waliokuwa wanasoma katika
Chuo Kikuu cha Garissa cha nchini Kenya kilichoshambuliwa na kundi la Al
Shabab na kuua watu 147.
Lowassa asali Ijumaa Kuu
Pia
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa,
amesema amani iliyopo nchini inapaswa kuenziwa kwa kuidumisha.
Kauli
hiyo aliitoa baada ya ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Askofu Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa,
katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam jana.
“Tushukuru
Mungu nchi yetu ina amani na Watanzania tuienzi amani kwa kuwa ndiyo
imesaidia hadi leo tunasherehekea Ijumaa Kuu kwa pamoja. Tuitumie amani
vizuri,” alisema Lowassa.
Naye,
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliyekuwepo katika misa hiyo
aliizungumzia Sikukuu ya Pasaka kuwa ni wakati wa kuonyeshana upendo.
“Tunaposherehekea
tuwasaidie wenye upungufu na hilo ndilo jambo kubwa ambalo ni upendo
mkubwa. Hii habari ya kusigana kwa namna yoyote katika dini zetu au
wakulima na wafugaji isiwepo,” alisema Sumaye.
Katika
ibaada hiyo Askofu Malasusa alilisihi taifa kuwa na unyenyekevu, utii
na upendo kama aliouonyesha Yesu Kristo kwa wanadamu.
Naye,
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu
Eusebius Nzigilwa, alisema kushamiri kwa vitendo vya kigaidi katika
mataifa mbalimbali duniani kunatokana na watu kukosa moyo wa upendo.
Akizungumza
jana wakati akiendesha ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Parokia ya
Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza, alisema hali hiyo inatokana na
kujengeka kwa chuki na uhasama ndani ya mioyo ya wanadamu katika miaka
ya hivi karibuni.
Kwa
upande wake, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Mchungaji
Samweli Mshana, amesema hatua ya NEC kusogeza mbele upigaji wa Kura ya
Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, kumewaondolea adha Watanzania kwa
kuburuzwa na Serikali.
Akizungumza
jana wakati alipohubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika
Kanisa la Usharika wa Dodoma mjini hapa alisema, kitendo kilichokusudiwa
na Serikali ni kutaka kuwaburuza Watanzania wapige kura ya ndiyo kwa
jambo ambalo hawalijui.
Alisema
wapo Watanzania wengi wanaotakiwa kupata elimu ya kutosha juu ya Katiba
Inayopendekezwa ili waweze kuwa na uhakika wa kile wanachokipigia kura
tofauti na ilivyokuwa sasa.
“Tuna
kila sababu ya kuipongeza NEC kwa uamuzi wa kuisogeza mbele kwa kuwa
baadhi ya viongozi wa Serikali wasiokuwa na nia njema na taifa hili
walitaka kutupeleka kama mifugo inayoenda kuchinjwa,”alisema Mchungaji Mshana.