Hakimu wa kesi ya mauaji ya Dk. Mvungi ajitoa
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waliarwande Lema, amejitoa kusikiliza kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, inayowakabili washtakiwa 11.
Tukio
hilo lilitokea juzi, baada ya washtakiwa hao 11 kumuomba Hakimu Lema
ajitoe kuisikiliza kesi yao ili iweze kupangwa kwa hakimu mwingine
ambaye wao wanaona atawatendea haki.
Kutokana
na ombi hilo, Hakimu Lema alijitoa na kuiahirisha kesi hiyo ambayo
upelelezi wake hadi sasa bado haujakamilika na itatajwa tena AprilI 20,
2015, itakapopangwa mbele ya Hakimu mwingine.
Mawakili
wa Serikali, Ofmad Mtenga na Diana Lukondo walidai kuwa upelelezi wa
kesi hiyo bado haujakamilika na waliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa
ajili ya kuitaja.
Miongoni
mwa washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi (32), John
Mayunga (56), Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa
(40), Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya (30), Ahmad Kitabu (30).
Washtakiwa
hao kwa pamoja wanadaiwa mnamo Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa la
mauaji kinyume cha kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura
ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.