Rais Kikwete Aombwa Kutoupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015 ....Ombi Hili Limetolewa Na Chama cha Bloggers Tanzania (TBN)
Mtandao wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN) tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni.
Muswada
wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na
matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na
kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa
kieletroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
Muswada Wa Sheria Ya Makosa Ya Mtandaoni,2015
Umoja
huu (TBN) ulishtushwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kukubali kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati
ya dharura kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado
ni kitu kipya nchini hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati
ya raia na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia
mitandao na yapi yanakubalika
Kimsingi
TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba
Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na
wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana
kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria
isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.
Hali
kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na
wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu
zenye uzito za kwanini sheria hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji
kwanini sheria hii ipite kwa dharura bila ya kupata majibu.
Muswada
huu ambao kati ya makosa mengi uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu
makubwa aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi kuwa na uwezo wa
kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la
uhalifu unaohusu mtandao. Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya
kumsulubisha mtuhumiwa katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho sahihi?
Mbali
na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia
maadili ya kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni kutunza usiri
wa chanzo cha habari yake pale inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi
kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo
vya habari.
Kupitia
sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini kutokana na kwamba sheria
inaainisha ni kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.
Aidha, tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013.
Muswada
huu unavinyima uhuru vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu
mbalimbali. Kama ilivyo Ibara ya 7(4) ‘‘Chombo chochote cha habari
ambacho kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au
kinatangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa
taarifa ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha
wananchi wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au
wasishirikiane na maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa.’’
Hii
inamaanisha kuwa hata blog zetu ziko hatarini kuelekea katika
kulazimika kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza takwimu
zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa
habari nchini.
Tunamkumbusha
mwananchi wa kawaida anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko salama
kwani sheria hii inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa taarifa za
wateja wake jambo ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea
habari.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
IMETOLEWA NA;
Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network-TBN)
04/03/2015.