Baada ya Gwajima kugeuka "Yuda" wa Lowassa....Dkt Slaa ajibu mapigo
Mchungaji wa kanisa la ufufuo na uzima,Josephat Gwajima amejitokeza hadharani na kukana kwamba hakuwahi kumuunga mkono Edward Lowassa wakati wa kampeni za Urais.
Akiongea katika mahojiano maalumu na kituo cha Azam Tv, Gwajima amesema yeye hakuwahi kuwa mshirika wa Lowassa wala chama chochote, bali aliitwa jijini Arusha na Jangwan Dar es Salaam kwa ajili ya maombi tu na sivinginevyo....
Amesema kitendo cha kukubali wito huo wa maombi kimewafanya watanzania wahisi kwamba yeye alikuwa team Lowassa, kitu ambacho sio kweli.
Amedai yeye alikuwa mfuasi wa mabadiliko ya nchi, alikuwa akiunga mabadiliko ya nchi na SIO personality ya mtu au chama cha mtu.
Wakati Gwajima akikana kumuunga mkono Lowasaa, kumbukumbu zinaonyesha kuwa mchungaji huyo alikuwa ni team Lowassa na alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha mheshimiwa Lowassa anashinda kiti cha Urais.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Gwajima alitumia nguvu kubwa sana wakati wa kampeni kupambana na Dr Slaa ambaye wakati huo alikuwa akishusha makombora mazito kuhakikisha Lowassa hashindi huku akimtuhumu Gwajima kuwa mshenga wa Lowassa aliyemfuata kumpigia debe wampokee Chadema
Tazama Video hii Kumsikiliza Gwajima
Baada ya Askofu Gwajima kusema kuwa hakuwa akimuunga mkono Lowassa, Dkt. Slaa amemtaka awaombe radhi Maaskofu pamoja na Watanzania kwa kuwadanganya.
Amesema hakutegemea Askofu Gwajima kumkana hadharani Lowassa
======Hili ni Tamko la Dr. Slaa======
i) Ni muhimu kwa "Mshenga Gwajima" kutubu na kuwaomba Radhi Watanzania kuliko kuendelea kuwapotosha.
ii) Mungu hamilikiwi na binadamu awaye yote. Watanzania tunawajibu wa kumshukuru sana Mungu kwa kutukomboa na kutuokoa na " Mabadiliko" ya " Kuzungusha Mikono". Mshenga na UKAWA yake walitaka kutuaminisha sote kuwa Mabadiliko ni kuzungusha mikono! Walitaka kutuaminisha kuwa "Mabadiliko ni Lowassa na Lowassa ni Mabadiliko".
Lowassa aligeuzwa kuwa "Ajenda" badala ya ajenda za Msingi za Wananchi. Mungu amesikiliza Sala za Wanyonge na Walalahoi. Namshukuru sana Mungu aliyenionyesha kuwa kati ya wawili hao, japo wote kila mmoja ana uchafu, Magufuli ni "Nafuu mara eflu" kuliko fisadi Lowassa. Asante sana Mungu Mwema kwa kulinusuru Taifa lako lililotaka kuingizwa "mjini" na makuwadi kwa ulaghai na upotoshwaji uliopitiliza.
iii) Nilimtaka Gwajima awaombe radhi Maaskofu aliosema "wamehongwa na Lowassa na kuwa fedha hizo waligawiwa mbele ya Mavho yake.
Alisema bila kumumunya maneno, kuwa.... Maaskofu wa ki lutheri alikwisha malizana nao" na kuwa kati ya "Maaskofu wa Kikatoliki 34 wamehongwa Maaskofu 30 na kumtaja kwa jina Askofu Mkuu mmoja, ambaye yeye kapewa fedha za kununulia gari la kiaskofu."
Fedha hizo alidai zimetolewa na Lowassa kupitia Rostam Azizi. Gwajima, Tambua kuwa kama ni kweli toka tena hadharani wakemee Maaskofu wanaopokea Rushwa, na kama si kweli Waombe Radhi hadharani Maaskofu hao kwani kauli hiyo ilitaka kuwagawa Maakofu na kuwachafua.
Lakini, alitamka hayo akiona ni sifa, ndiyo maana nilimshangaa kiongozi wa dini ambaye badala ya kukemea anaona ni sifa. Kama wenzangu waliokuwepo na wao wana Misingi ya kusimamia basi watatoa ukweli wao, na kama wanachukia ufisadi basi watatoka hadharani kukemea tamko hilo lililotolewa mbele yetu watu 4 akiwemo Mshenga.
Nilipotamka hivi wengi walidhani Dr. Slaa ndiye Katamka kuwa Maaskofu "Wamehongwa". Kama Askofu anaweza kufika mahali akawasingizia wenzake ni hatari sana na halihitsji kufungiwa Macho na masikio.
Kama anavyosema Gwajima ni " kweli". Basi wote tunaopenda kupiga vita Ufisadi ni lazima tupaze sauti zetu, na kukemea kitendo hicho kama kweli kimefanywa na wale tunaotegemea kusimamia maadili katika Jamii yetu.
Wako walioniambia Dr. Slaa unapata wapi ujasiri wa kuwasema viongozi wa dini. Sijawahi kuyumba wala kuyumbishwa. Ukweli utatamkwa hata kama ni mchungu, na uovu na uozo utasemwa tu hata kama umetendwa na nani. Ukitazama nyuso za wazi " haki haitatendeka milele.
iv) Katika busara ya kawaida, hatukutegemea Gwajima kujitokeza "Kumkana Lowassa" hasa kabla ya kuomba radhi. Aidha Kauli " Live" kwenye YouTube na mitandao mbalimbali ziko bado kibao. Ama kweli Gwajima ni kiongozi asiye na dhamira kukanusha kauli zake hizo kabla ya kuomba radhi.
v) Wako watakaodhani kuwa Dr Slaa ana "bifu" binafsi na Gwajima. Ni kweli kibinadamu nimeumia sana kwa kuwa kuumizwa na rafiki kunaumiza sana, lakini nawaonea huruma zaidi Watanzania Waliobebwa kwa ushabiki mkubwa na kupoteza nguvu zao nyingi na labda "kupoteza fursa ya kuiondoa CCM kwa muda mrefu ujao" kwa kuwaamini watu kama kina Gwajima. Hiki ndicho kinachonisukuma zaidi kuendelea kumkaba Gwajima hadi atakapoomba radhi kwa watanzania wanyofu.
Nawaomba Watanzania tuwe na kumbukumbu. Tuzisikilize tena Kauli mbalimbali alizozitoa Gwajima, tena wakati mwingine kwa njia ya Maombi kwa jina la Mungu. Hali hii isipokemewa kwa ukali sana ni hatari sana.
Ndugu watanzania wenzangu,pamoja na yote haya, ninawatakia Heri nyingi kwa sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya 2016 uwe wa Baraka na mafanikio.
-Dk Willibrod Slaa-