IGP apangua jeshi la polisi


Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu amelifumua Jeshi la Polisi nchini kwa kupanga na kupangua vigogo wake, huku baadhi wakipandishwa nyadhifa.


Pangapangua hiyo imewagusa pia maofisa waandamizi wa jeshi hilo walioko makao makuu, makamanda wa mikoa, wakuu wa upelelezi wa mikoa (RCO) na wakuu wa polisi wa wilaya (OCD).


Habari za uhakika kutoka ndani ya makao makuu ya Jeshi la Polisi zinasema pangapangua hiyo imewagusa pia wakuu wa vikosi, wakuu wa polisi wa vituo (OCS) na polisi wa vyeo cha chini.


Akizungumza jana, msemaji wa polisi, Advera Bulimba alisema: “Mabadiliko hayo ni ya kawaida ya ndani, hayana uhusiano na kasi ya Rais John Magufuli ila kazi lazima ifanyike.”


Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kukutana na maofisa wa polisi kwenye Bwalo la Maofisa wa jeshi hilo Oysterbay jijini Dar es Salaam na kati ya mambo yaliyotajwa ni kukumbushana utendaji, uwajibikaji na mpango wa kulifumua jeshi hilo.


Chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kimedokeza kuwa orodha ya waliokumbwa na pangapangua hiyo ni ndefu .


“Nafikiri IGP ameamua kusuka upya safu ya uongozi ili kuboresha ufanisi katika utendaji wa kazi. Unajua jeshi lazima liendane na falsafa ya Rais Magufuli (John) ya Hapa Kazi Tu,” alidokeza afisa mwingine.


Mabadiliko hayo yamekuja wakati tayari makamanda wa polisi wa baadhi ya mikoa wakiwa wamebadilishwa katika vitengo walivyokuwa awali, wakiwamo Kikosi cha Usalama Barabarani, ili kuboresha utendaji wa jeshi hilo.


Katika mabadiliko hayo, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Salehe Ambika amehamishwa kutoka kitengo cha Sheria na Huduma za Utafiti kwenda kuwa mkuu wa utawala.


DCP Robert Boaz amehamishwa kutoka kitengo cha intelijensia kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha uhalifu wa kitaifa na uhalifu wa kupangwa au Transnational and Organized Crime (TOC).


Katika panguapangua hiyo, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Luteta Modest amehamishwa kutoka kitengo cha sheria kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha sheria na huduma za utafiti.


Mkoa wa Kilimanjaro umetikiswa zaidi na mabadiliko hayo baada ya maofisa watano waandamizi kuhamishiwa vituo vipya na nafasi zao kuchukuliwa na sura mpya.


Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Fulgence Ngonyani amehamishiwa Chuo cha Polisi Kilwa Road, na RCO Ramadhan Ng’anzi amehamishiwa mkoa wa Shinyanga kuendelea na wadhifa huo.


OCD wa Moshi, Mrakibu Mwandamizi Deusdedit Kasindo amepanda cheo na kwenda kuwa kamanda wa Mtwara, wakati mkuu wa kitengo cha FFU wa mkoa huo, amehamishiwa mkoa mwingine.


Katika mabadiliko hayo, kamanda wa mkoa wa Iringa, Kamishina Msaidizi Ramadhan Mungi amehamishiwa Kilimanjaro kuchukua nafasi ya Ngonyani anayekwenda chuoni.


Nafasi ya RCO wa Kilimanjaro imechukuliwa na SSP Black Magesa aliyekuwa OCD Korogwe.


Kamanda wa Mkoa wa Manyara, ACP Christopher Fuime amehamishiwa Kinondoni kuendelea na wadhifa huo, wakati kamanda wa Ruvuma, ACP Mihayo Miskhela amehamishiwa mkoani Tanga.


Pia, kamanda wa Mkoa wa Tanga, ACP Zuneri Mumbeki amehamishiwa Ruvuma kuendelea na wadhifa huo, huku kamanda wa Kinondoni, SP Camilius Wambura amehamishiwa Mkoa wa Manyara kushika wadhifa huo.


Maofisa wengine ni Gerald Ngichi, ambaye alikuwa OCD Magomeni, amehamishiwa Lindi, Nsekela M. Nsekela (OCD Nyang’wale sasa ofisa mnadhimu II Rorya, Nesto Msembele (OCD Mbalizi sasa Polisi Jamii Mbeya), William Malei (ofisa mnadhimu ll Kigoma, sasa OCD Korogwe), Melard Sindano (OCD Kigoma, sasa OCD Nyang’wale).


Wengine ni Patrilinius Mlowe (OC-CID Kwimba, sasa OCD Kawe, Edson Kasekwa (OCD Makambako, sasa OCD Kilolo), Agustino Titus (mnadhimu ll Morogoro, sasa OCS Malinyi).


Katika pangua pangua hiyo, Raphael Msela (ofisi ya RCO Kagera, sasa naibu RCO Kagera), John Samwel (OCS Malinyi, sasa ofisa mnadhimu II Morogoro), SP Debora Mrema (polisi jamii Mbeya, sasa OCD Mbalizi, SP Omari Mtungu (OCD Tanga, sasa OCD Moshi),SP Alfred Mwaikusa ambaye alikuwa OCS Singida sasa anakwenda kuwa OC-CID Serengeti.


Wengine ni SP Limited Mhongole ambaye alikuwa OC-CID Mbarali sasa anakuwa OCD Mbarali, ACP Jaffar Mohamed (RPC Pwani, sasa makao makuu) na ACP Peter Kakamba anakuwa RPC Iringa.

Pia ACP Mussa Taibu aliyekuwa RCO Shinyanga, sasa anapelekwa upelelezi makao makuu, SSP Pili Omari (OCD Kawe, sasa OCD Mwanga, David Chidingi (OCD Lindi, sasa OCD Magomeni, SSP Constantiono Mbugambi (OCD Mwanga, sasa OCD Ngara), SSP Jullius Lukindo (OCD Mbarali, sasa OCD Mvomero).

ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini