Yanga yatangaza kuachana na Niyonzima, yampiga faini Dolla 71,175




Na Rabi Hume, Modewjiblog

Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imetangaza kuachana na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima (pichani) kutokana na mchezaji huyo kuvunja masharti ya mkataba na kuwa na utovu wa nidhamu.

Akitangaza uamuzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema Niyonzima ameshindwa kufuata makubaliano ya mkataba aliyowekeana na klabu hiyo kwa kuvunja kanuni za mkataba alioingia na Yanga.

Muro alisema kuwa Niyonzima amekuwa na tabia ya kuondoka klabuni kwenda kujiunga na timu ya taifa ya Rwanda bila kuomba ruhusa kwa uongozi na hata wakati wa kurudi huwa anachelewa kuripoti hali inayopelekea kuvuruga baadhi ya programu za mwalimu wa klabu hiyo.

Muro aliongeza kuwa baada ya kumalizika kwa mashindano ya Cecafa Senior Challenge, Niyonzima hakurejea klabuni na ndipo alipoitwa na kamati ya maadili ya klabu ili atoe maelezo kwanini amechelewa kuripoti na alikiri kufanya kosa hilo hivyo kutakiwa kutoa maelezo kwa maandishi ambayo siku ya mwisho kupokelewa ilikuwa ni Disemba, 23 lakini hakufanya hivyo.

“Tukio ambalo amefanya Niyonzima nilakutokusheshimu mkataba na utovu wa nidhamu, ameitwa na kamati kutoa maelezo akakiri kuwa na kosa akaambiwa aandike kwa maandishi lakini hajafanya hivyo na hivyo kukiuka masharti ya mkataba na sasa rasmi tunatangaza kuvunja mkataba na Niyonzima,” alisema Muro.

Muro aliongeza kuwa baada ya kuvunja mkataba na mchezaji huyo wanamtaka awalipe kiasi cha Dola 71,175 amabzo ni zaidi ya Milioni 140 za kitanzania kwa ajili ya gharama na makubaliano ambayo walikubaliana katika mkataba wa Niyonzima ambao ungemalizika 2017.

Aidha mkuu huyo wa kitengo cha mawasiliano alisema kama kuna klabu yoyote itataka kumsajili Niyonzima kabla ya mchezaji huyo kulipa pesa hizo wataweka pingamizi la usajili huo kwa kutumia kanuni namba 17 na kifungo kidogo cha pili cha kanuni za Shirikisho la Soka Duniani FIFA ambayo hairuhusu klabu yeyeto kusajili mchezaji ambaye bado hajamalizana na klabu aliyokuwa akiitumika.

Alisema klabu inayomtaka Niyonzima wafanye nae mazungumzo na waone kama wanaweza kumsaidia kulipa kiasi hicho cha fedha na baada ya hapo atakuwa huru kuitumikia klabu yoyote atakayotaka kuchezea.

ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …