Mchawi akamatwa akiwa uchi huko Simiyu
JESHI la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mkazi wa Lamadi, Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, Grace Ndimishinji (36), kwa tuhuma za kukutwa akijihusisha na ushirikina katika Kijiji cha Lamadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gemini Mushy, alisema tukio hilo ni la kipekee kutokea katika Mkoa huo ambapo mtuhumiwa alikutwa uchi wa mnyama asubuhi kwenye familia ya Yusta Thomas (35).
Alisema mtuhumiwa alikutwa jikoni Desemba 22, mwaka huu akiwa amening'inia bila kujitambua ambapo mama mwenye nyumba baada ya kumuona, alipiga kelele akiomba msaada kwa majirani," alisema.
"Siku ya tukio, mume wa Yusta ambaye ni mfanyabiashara wa samaki hakulala nyumbani... alipofika nyumbani alilikuta tukio hilo, alimwamuru mama huyo ashuke chini alikokuwa amening'inia akiwa uchi, wakati huo polisi walifika eneo hilo, kumvisha nguo, kwenda naye kituoni. Mtuhumiwa anaendelea kufanyiwa uchunguzi ambao ukikamilika, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ushirikina," alisema.
Kwa upande wake, Yusta alisema saa nane usiku, alisikia sauti za watu wakiitana majina bila kuwajua akina nani lakini wakati huo mbwa wao alipobweka, watu hao waliacha mazungumzo na kunyamaza.
"Mwanangu wa kike aliniambia kuna watu wanazungumza nje ya nyumba na walipoamka asubuhi walimkuta mtuhumiwa akining'inia jikoni na kuomba asamehewe akidai dereva wake amemwambia ashuke pale atampitia.
"Mtuhumiwa alikuwa amebeba kiberiti kisichokuwa na njiti, majaribu ya kimiujuza yamekuwa yakijitokeza katika nyumba yetu mara kwa mara lakini tukio hilo liliwashangaza sana," alisema.
Alipoulizwa ni vitu gani vilivyochangia mama huyo anase nyumbani kwake na utaalamu gani waliotumia kumshusha, Yusta alidai ni maombi pekee kwani tangu alipoanza kusikia minong'ono nje alianza kuomba.
Baadhi ya majirani walisema tukio hilo ni la kipekee na litasababisha watumishi wa idara mbalimbali kutofika Busega wakihofia vitendo vya kishirikina na kuitaka jamii ibadilike, kuachana na imani hizo.
Tukio hilo ni la pili kutokea wilayani humo ambapo Septemba 3, 2014 huko Bushigwamhala, Kata ya Kalemela, watu wanne wa familia moja walikutwa asubuhi wakilima uchi wa mnyama shambani kwao wakiamoni mahindi yao yatatoa mavuno mengi.