Matatizo yanayowafanyawaugue mara kwa mara
Watoto wanaopatwa na matatizo ya kuugua mara kwa mara ni wale walio katika umri wa chini ya miaka mitano. Watoto hawa huumwa na wanapogundulika kuwa ni wagonjwa tayari hali inakuwa mbaya.
Hii ni kwa kuwa watoto hawa hawana uwezo wa kujieleza mara tu wanapopata dalili za awali za ugonjwa. Pamoja na yote, magonjwa au maradhi ya watoto huanzia mbali sana kama tutakavyokuja kuona.
Inawezekana kabisa mtoto asiugue na akaishi vizuri kuanzia anapozaliwa hadi anavuka umri wa miaka mitano. Matatizo mengi ya kiafya kwa watoto hupunguza umri wao wa kuishi au huwadhoofisha kimwili na kiakili na kusababisha wasikue vizuri na hata uwezo wao wa kujifunza mambo mbalimbali ya kimaisha katika familia au darasani hupungua.
Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali katika jamii nyingi hapa Afrika Mashariki, watoto wapo kwa idadi kubwa kuliko watu wazima na inakadiriwa watoto ni asilimia 50 ya watu wazima lakini watoto 250 kati ya 1000 wanaozaliwa hufariki kabla hawajasheherekea bethidei yao ya kutimiza miaka mitano. Hali hii kitaalamu huitwa ‘Underfive Mortality’.
dadi hii ya vifo vya watoto inaweza kupungua au kutofautiana katika jamii mbalimbali kutegemea na uboreshwaji wa huduma za afya ya msingi, lishe na malezi bora ya watoto.
VYANZO VYA MATATIZO YA AFYA KWA WATOTO
Vyanzo vya matatizo ya kiafya kwa watoto walio chini ya miaka mitano vipo vingi lakini kimsingi tunayaweka katika makundi matano;
Kundi la kwanza ni la watoto walio na umri wa chini ya mwezi mmoja ambao ndiyo kwanza wamezaliwa hadi wanafikisha siku 30. Watoto hawa huathirika zaidi na matatizo wanayopata wakati wanapozaliwa.
Hapa inahusiana zaidi na hali halisi ya mama wakati wa ujauzito hadi uchungu ndiyo maana inashauriwa mama aanze kliniki mara moja anapohisi tu kuwa ni mjamzito na ajifungulie hospitali.
Hii itasaidia kukabiliana na matatizo ya uzazi mapema kabla hayajaleta madhara. Hali nyingine ni mtoto kuchelewa kulia mara tu baada ya kuzaliwa, mtoto kuzaliwa njiti au uzito mdogo, uzito mzuri ni zaidi ya kilo mbili na nusu, mtoto kuzaliwa na kasoro toka tumboni mwa mama, mtoto kuwa na homa kali mara tu baada ya kuzaliwa, kupata pepopunda kutokana na kitovu chake kuchelewa kupona. Kitovu kinakauka kabisa ndani ya siku saba tangu kuzaliwa.
Kifo cha mama mzazi wa mtoto, yaani mama kufariki kwa tatizo lolote mara tu baada ya kujifungua na kumuacha mtoto bado mchanga kukosa lishe na matunzo mazuri, hivyo mtoto anaweza kudhoofika kiafya, kukosa lishe, kuharisha na hata kupoteza maisha.
Kundi la pili ni la watoto walio katika umri wa chini ya mwaka mmoja, yaani mwezi mmoja hadi mwaka hawa kitaalamu tunawaita ‘Infancy’ na wale walio na umri chini ya mwezi mmoja tunawaita ‘Neonates’.
Watoto hawa ‘Infants’ hukabiliwa na magonjwa ya njia ya hewa, mfano homa ya mapafu au nimonia, kifaduro na mengineyo.
Husumbuliwa pia na kuharisha mara kwa mara kutokana na kunyonya kwa kutumia chupa au nyonyo na kula vyakula visivyofaa mfano kuwachanganyia vyakula vinavyoiva tofauti, wengine huita ‘Lishe’, mtoto kupewa chakula kwa kipindi chini ya miezi sita na kumkatisha maziwa ya mama au kumpa maziwa ya ng’ombe katika umri wa chini ya mwaka mmoja.
Watoto hawa pia husumbuliwa na homa ya malaria mara kwa mara kama chandarua hakitatumika kikamilifu na mazingira hayataboreshwa husababisha mbu kuzaliana. Mtoto anaweza kuugua surua kama hatapata chanjo kwa muda muafaka anapotimiza miezi tisa.
Yote haya yanaweza kusababisha mtoto akapata utapia mlo.
Kuanzia umri wa miaka miwili hadi mitano, mtoto anaweza kupata utapia mlo na kwashakoo.
Itaendelea wiki ijayo.