INATISHA SANA! MWANAJESHI AUA MKEWE KWA SHOKA, NAYE AJIUA HUKO MWANZA!

Picha na maktaba ila siyo ya tukio hilo!
Mashaka baltazar, Mwanza 
ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jacob Mponeja wa kikosi  cha 512  MCT Nyegezi, Mwanza, anadaiwa kumuua mkewe kwa kumkata na shoka kichwani kisha mwenyewe kujinyonga hadi kufa chumbani kwake, tukio lililotokea mwanzoni mwa wiki hii jijini Mwanza. 

Habari kutoka kwa watoto wa marehemu zinasema, kabla ya tukio hilo, wanandoa hao walikuwa na ugomvi unaodaiwa ulitokana na wivu wa kimapenzi. Mmoja wa watoto wa marehemu, Sara Mponeja, akizungumza na waandishi wa habari, alisema marehemu  mama yake awali alikuwa safarini Bariadi mkoani Simiyu, ambapo alirejea nyumbani  Ijumaa wiki iliyopita. 

Alisema baada ya kurejea, alikuta ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ katika simu ya baba yao ndipo ugomvi baina yao ulipoanza.“Hali hiyo iliendelea na juzi usiku baada ya chakula kuandaliwa, baba aligoma kula, ndipo mama naye alikataa kula. Wakati tumelala, tulisikia kelele za ugomvi, ingawa mwanzoni tulichukulia ni hali ya kawaida. Asubuhi tulishangaa mlango wao haufunguliwi. 

“Si kawaida kufika saa moja mama hajaamka, nilienda kugonga mlango, sikujibiwa, kuchungulia nikaona mama amelala chini ndipo niliporudi kwenda kumweleza kaka yangu  Paulo.“Kaka alilazimika kupanda juu ya dari na kuchungulia ndani ndipo akamuona baba amejitundika na mama akiwa amelala sakafuni huku akikoroma, damu zimetapakaa, akapiga kelele zilizowaleta majirani ambao waliamua kuvunja mlango. 

“Polisi walifika na kumchukua mama na kumkimbiza Hospitali ya Rufaa Bugando, lakini ilipofika saa 7:00 mchana alifariki dunia,” alisema na kuhitimisha kwa kusema kuwa mwili wa baba yake pamoja na shoka ulichukuliwa na polisi. 

Mwenyekiti wa mtaa wa Igubinya, Costantino Kalemela, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa alikuta ujumbe mfupi ndani ya nyumba ya marehemu hao, ulioandikwa na askari huyo ukieleza  chanzo cha kifo chake kuwa ni ushirikina wa mkewe na wivu wa mapenzi.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Valentino Mlowola (pichani), simu yake iliita bila kupokelewa.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini