Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini

Wanafunzi wa shule za msingi mkoani Geita wamewalalamikia walimu wao kufanya kazi migodini na kuendesha bodaboda, hali inayosababisha wafeli kutokana na kutofundishwa darasani.
Hata hivyo, Ofisa Elimu, Mkoa wa Geita, Eufransia Buchuma alisema juzi kuwa walimu hukimbia vipindi hali inayodhorotesha ufaulu.
“Tumeweka mikakati kwa kila walimu wakuu wote kutoa taarifa kuhusu watakaoshindwa kuhudhuria vipindi au kuwa watoro, kisha hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu za kazi,” alisema Buchuma.
Wakizungumza hivi karibuni, baadhi ya wanafunzi walisema hawamalizi silabasi kutokana na walimu kutokuwapo kwani siku nyingine wanarudi nyumbani bila kusoma.
“Walimu hawafundishi, mnaweza kukaa wiki nzima bila mwalimu kuingia darasani, siku nyingine zote haumuoni au anakuja kusaini kisha anaondoka,” alisema mwanafunzi Retias Devid.
Alisema walimu wengine wanafanya shughuli zao migodini, hivyo mwitikio wa kufundisha unakua mdogo.
“Hata wakifundisha hawafundishi kwa moyo jambo linalotuathiri wanafunzi na kusababisha kufanya vibaya katika masomo yetu.
“Kwa kweli hii hali inasababisha wengine waache shule” alisema Sebastian Kauzeni.
Pia wanafunzi hao walisema wamekuwa wakipata changamoto ya walimu kusitisha vipindi na kwenda mjini kufuatilia mishahara yao.
“Mwalimu anaweza akaondoka shuleni siku mbili yuko mjini kufatilia mishahara benki, tunakuja shule na kuishia kucheza tu, mnaweza kufululiza hata wiki nzima mwalimu hayupo,” alisema Catheline Masaru.
Baadhi ya walimu wao walikiri kuwapo kwa hali hiyo kutokana na masilahi yao kuwa madogo.
“Sisi walimu tunashida sana, ukisema ufanye kazi za ualimu tu utakufa maskini, kama unavyojua masilai yetu ni madogo na hayaji kwa muda mwafaka...unakuta unafuatilia madai yako mwaka mzima,” alisema Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyankumbu, Christina Moses.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama