HII NDIYO A - Z YA BINTI MCHAWI ALIYEDONDOKA KWA CHUNGU KUTOKA ANGANI MJINI SHINYANGA


Mfano wa usafiri waliotumia kufika eneo la tukio japokuwa yeye anadai alikuja na usafiri wa Chungu


Katika hali isiyokuwa ya kawaida binti anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 23- 25 anayedaiwa kuwa ni mchawi amekutwa kwenye nyumba ya mtu katika mtaa wa Bushushu kata ya Lubaga katika manispaa ya Shinyanga akiwa amevaa kishirikina na mwili wake ukiwa umepakwa dawa nyeusi akidai alikuwa anaongoza wenzake zaidi ya 10 kutoka kanda ya ziwa kuwanga katika nyumba hiyo.

Tukio hilo lililovuta hisia za mamia ya wakazi wa Shinyanga limetokea jana asubuhi nyumbani kwa Robinson Massawe ambapo binti huyo alikutwa amelala mbele ya mlango wa nyumba hiyo akiwa hajitambui na baada ya kusemeshwa ndipo akasimulia yaliyomkuta kwamba alifika mahali hapo na wenzake zaidi ya 10 kufanya sherehe baada ya kufanikisha uchawi wao.

Mashuhuda wa tukio walisema baada ya kumhoji binti huyo alisema alifika kwenye familia hiyo,akiwa kiongozi wa kundi la wachawi zaidi ya 10 kutoka Ushirombo,Misungwi na Shinyanga saa 9 usiku kwa ajili ya kufanya sherehe baada ya kufanikiwa kusambaratisha kichawi ndoa ya Massawe na Mary Joseph.

“Tumemkuta hapa anasema leo ni mara ya tatu wanakuja kufanya uchawi wao,lengo lao ni kutaka ndugu yao aolewe na Massawe,walikuja siku ya kwanza wakakuta mke wa Massawe akisali,wakashindwa,wakarudi mara ya pili kwa ajili ya kusambaratisha ndoa,wakafanikiwa leo walikuja kufanya sherehe kwa kazi hiyo lakini wenzake wamemkimbia”,alieleza Stella Joseph mdogo wa mke aliyeachika.

“Anadai kuwa Robinson alitoa ahadi ya kumuoa mwanamke ambaye ni ndugu yao badala yake akaoa mwanamke mwingine,aliyeahidiwa kuolewa katoa taarifa kwa mama mdogo wake ambaye ni mchawi,naye kalifikisha kwa wakuu wake,wakaamua kuingia kazini kutaka ndoa kishirikina”,aliongeza Hamis Juma.

Akizungumza na Malunde1 blog iliyofika eneo la tukio haraka sana tena  kawaida yake,binti huyo anayedaiwa kuwa mchawi aliyejitambulisha kwa jina la Coletha akizugumza kwa lugha ya Kisukuma kutoka Ushirombo mkoani Geita, alisema alikuwa anaongoza kundi la wachawi kutoka Mwanza,Geita na Shinyanga lakini wakazidiwa nguvu wenzake wakamkimbia.

“Mimi ni mdogo sana kwa wachawi wenzangu,siyo mzoefu sana,walinitanguliza mbele ,nilipodondoka na chungu change wenzangu wakanikimbia,nimebaki peke yangu,kila mmoja amekuja na usafiri wake,mimi nimekuja na chungu,wengine wamekuja na ungo”,alieleza Binti huyo.

"Baba mwenye nyumba hii alitoa ahadi ya kuoa mtoto wa mshirika mwenzetu(mama mdogo wa binti),na mama mdogo huyo ndiyo akaleta malalamiko kwa wachawi kuwa tumshughulikie huyu baba anayechezea watoto wa watu",aliongeza.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Bushushu Ruben Masanja aliyefika eneo la tukio alisema ni kweli ndoa ya Robinson na Mary imevunjika tangu mwezi Septemba mwaka 2014 na sasa baba wa familia hiyo anaishi na ndugu zake.

Masanja aliongeza kuwa huenda binti huyo ni mchawi kutokana na maelezo yake na vitendo vilivyotokea katika familia hiyo huku akiwasihi wakazi wa eneo hilo kutomwadhibu binti huyo kisha kumwingiza ndani ya nyumba kusubiri polisi kwa ajili ya usalama wake.

“Anasema walikuja kufanya sherehe baada ya kumaliza kazi ya kuvuruga ndoa,na kweli wanandoa wametengana tangu tarehe 17 Septemba 2014,sasa wachawi hao wanataka ndugu yao aliyeahidiwa kuolewa na Robinson aolewe,binti anayetaka kuolewa alitoa taarifa kwa mama mdogo wake ambaye ni mchawi,huyo mama akatoa taarifa kwa wachawi wenzake ili washughulikie suala hilo”,Masanja aliiambia Malunde1 blog

Hata hivyo katika hali ya kushangaza watu mwanzo kufika katika eneo la tukio walitoweka na vipande vya chungu alichodondoka nacho binti huyo.

Kufuatia tukio hilo askari wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga walifika eneo la tukio na kumchukua binti huyo kwenye gari la polisi.

Tukio hili la binti kukutwa akiwanga nyumbani kwa mtu limetokea siku chache tu baada ya bibi asiyejulikana makazi yake mwenye umri wa miaka 80 kukutwa uchi nje ya nyumba ya mtu katika kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga.
Na Kadama Malunde-Shinyanga 



Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini