Kituo kingine cha polisi chavamiwa.....Majambazi Yapora Bunduki, Risasi 30 na vitu vingine kibao



Kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia na kuvunja stoo ya Kituo kidogo cha Polisi Mngeta, Kilombero na kuiba bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.
 
Majambazi hao pia wanadaiwa kuiba jenereta, redio, viti, betri ya gari na spika ya redio.
 
Akizunguzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema uporaji huo ulitokea usiku wa Februari Mosi.
 
Kituo hicho ni cha tatu kuvamiwa mwaka huu baada ya Kituo Kikuu cha Polisi Rufiji, Mkoa wa Pwani na Bukombe kuvamiwa na majambazi na kuua polisi wawili na kupora bunduki saba na risasi 60.
 
Mwaka jana majambazi walivamia Kituo cha Polisi Mkamba, wilayani Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo wawili kisha kupora bunduki tano na risasi 60.
 
Kadhalika, Juni mwaka jana, majambazi yalivamia Kituo cha Polisi Bukombe na kuua askari wawili na kupora bunduki 10 na risasi kadhaa.


Akizungumzia uvamizi huo, Kamanda Paulo alisema baada ya wizi huo askari walianza msako na kufanikiwa kuipata bunduki hiyo na risasi 30, viti vitatu, jenereta na redio vikiwa vimefichwa katika pori la Simbangingile lililopo Mngeta Wilaya ya Kilombero.
 
Polisi inawashikilia watu watatu kutokana na tukio hilo ambao ni Ramadhani Shewele (20), Hamisi Ahmed (45) na Ignus Shewele (34) wote wakazi wa Nakagulu.
 
Alisema mtuhumiwa mmoja aliyetajwa kwa jina la Emmanuel Shewele (41) bado anatafutwa na polisi.
 
Kamanda Paul aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kuwapata watuhumiwa wengine.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini