KWA NINI WATU WENGI HAWAFANIKIWI MAISHANI?- 8
NI matumaini
yangu kwamba msomaji wangu unaendelea vizuri na kazi ya kulisukuma mbele
gurudumu la maendeleo kupitia ujasiriamali. Mada tunayoendelea
kuijadili ni sababu zinazofanya watu wengi washindwe kufanikiwa.
Wiki
iliyopita, niliishia kueleza kwamba watu wengi hawafanikiwi kwa sababu
hawawezi kuwa mabahili katika matumizi ya pesa wanazozipata. Niliishia
kukupa mfano wa jinsi mimi na dada yangu tulivyokuwa na hulka tofauti za
matumizi ya pesa tulipokwenda kwenye mashindano ya Umiseta mjini
Songea.
Kabla sijaendelea mbele, ningependa kumalizia mfano huo:
Mzee wetu
alitupatia Sh. 5,000 kila mtu kama ‘pocket money’ na pesa ya kutumia
njiani wakati wa safari. Kwa wakati huo ilikuwa ni pesa nyingi sana kwa
mwanafunzi. Pengine kwa nyakati hizi ingekuwa ni zaidi ya shilingi laki
moja.
Cha kushangaza
ni kwamba, mara baada ya kufika tu Songea ambako tulipaswa kukaa kwa
wiki moja kamili mimi nilianza kutumia ile pesa hovyohovyo kama vile
kununua chips kuku, soda za mara kwa mara pamoja na marafiki, kwenda
muziki n.k.
Baada ya siku
mbili tu, nikawa nimeishiwa kabisa. Sasa kumbuka mwaka 1992 shilingi
5000 ni pesa nyingi sana. Baada ya hapo nikawa sina ujanja zaidi ya
kwenda kucheki na dada Mary kama yeye alikuwa bado na kiasi ili
anikopeshe.
Kilichonishangaza
ni kwamba Mary alikuwa hajatumia hata senti moja katika ile 5000/-
yake! Wow! Hilo jambo lilinishangaza kupita maelezo ya kawaida. Hivyo
ilikuwa wazi kwamba mimi nilikuwa mfujaji wakati dada yangu alikuwa
mtunzaji. Je, wewe ni mfujaji au mtunzaji?
Wakati mwingine
ambapo somo hili lilijirudia vizuri sana, ilikuja kuwa takriban miaka
13 baadaye. Mwaka 2005 nikiwa kwenye ajira zangu za mwisho mwisho kabla
sijajiajiri, nilikuwa nafanya kazi kama ofisa mauzo wa Apsi Business
Manager jijini Dar es Salaam. Kampuni ilikuwa ndogo ya wastani yenye
watu kama 10 hivi pamoja na wakurugenzi wake.
Lakini kulikuwa
na kijana mmoja aliyekuwa mesenja pale ofisini kwa jina la Jose. Mara
kwa mara, baada ya sisi sote wafanyakazi (kasoro wakurugenzi kuishiwa)
tulikuwa tunakimbilia kwa Jose kumuazima pesa. Pamoja na kwamba Jose
alikuwa na mshahara mdogo kuliko wote, lakini ndiye aliyekuwa na
udhibiti mkubwa wa pesa kuliko sisi maofisa wengine wote! Ni ajabu sana.
Hivyo,
haijalishi unalipwa kiasi gani cha pesa kila siku, wiki au mwezi,
inajalisha unaweza kutunza kiasi gani cha pesa hiyo. Kwa hivyo weka
malengo ya kudhibiti pesa yako leo ili uanze kuchangisha kwa ajili ya
mtaji wako wa biashara au kwa ajili ya mambo ya msingi zaidi maishani.