Mdee amfunika Magufuli
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(BAWACHA), Halima Mdee, amebomoa ngome ya mbunge wa Chato, Dk. John
Magufuli kwa kuzoa wanachama zaidi ya 300 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
akiwa katika ziara yake wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, amejizolea umaarufu mkubwa
nchini kiasi cha kujijengea taswira kwamba anaungwa mkono jimboni kwake,
ambapo sasa kwa pigo hilo la Mdee, atapaswa kujipanga upya.
Akiendelea na ziara yake ya Kanda ya Ziwa ya kuimarisha chama na
kuhamasisha wananchi waikatae Katiba mpya inayopendekezwa, Mdee
aliwapokea wanachama hao wa CCM na kuwakabidhi kadi za CHADEMA kwenye
mkutano wa hadhara uliyofanyika juzi katika viwanja vya stendi ya
zamani.
Wanachama hao walieleza kuwa sababu iliyowasukuma kukihama chama hicho
ni kutokana na kuchoshwa na kauli za kejeli za mbunge wao, Dk. Magufuli
kila wanapomhoji kuhusu utekelezaji wa ahadi zake.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Christopha Masanja alisema kuwa
wanakabiliwa na kero nyingi ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama licha
ya kuwa karibu na ziwa Victoria, lakini kila wanapojaribu kumweleza
mbunge wao, huishia kuwapa kauli za kejeli.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi, Mdee alisema kuwa serikali ya CCM
imekuwa haiwathamini wananchi wake ndio maana imeshindwa kutoa
kipaumbele kinachostahili katika kutatua kero zao na badala yake
kuelekaza fedha nyingi kwenye mambo yasiyo na msingi.
Alisema kuwa sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa Watanzania zaidi ya
aslimia 80 imetengewa kiasi kidogo cha fedha kwenye bajeti ya mwaka huu
ya sh. bilioni 42 huku safari za rais zikitengewa sh. bilioni 50.
ya sh. bilioni 42 huku safari za rais zikitengewa sh. bilioni 50.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, aliwataka wananchi wa Chato kufanya
mabadiliko na kuondoa uteja kwa CCM akisema kuwa licha ya kuwapa kura
tokea nchi ipate uhuru lakini wameshindwa kuwatatulia kero zao.
Aliwataka kutorudia makosa hayo kwenye chaguzi zijazo badala yake
wahakikishe kwenye ngazi zote za uwakilishi wanachagua wagombea
watakaosimamishwa na CHADEMA.
Chanzo: Tanzania Daima.