Si Chid Benz tu, Uteja wa Madawa ya Kulevya Bongo Flava Upo Hivi
Ni
matunda ya saikolojia mgeuko, au unaweza kuita saikolojia kinyumenyume
(reverse psychology). Yanayokatazwa yanavutia zaidi watu kuyatenda.
Hakuna mtu ambaye hajui athari za matumizi ya madawa ya kulevya lakini
kuna watu huwaambii kitu.
Madawa ya kulevya ni sumu, ni kifo, inatangazwa hivyo leo, yule aliyekuwa anasikiliza tangazo, kesho anaanza kutumia. Hiyo ndiyo inaitwa reverse psychology, na mara nyingi huwasumbua sana vijana, maana damu inachemka, nguvu ya mwili inawadanganya.
Unadhani wakati Rehema Chalamila ‘Ray C’ anaanza kutumia ‘unga’ alikuwa hajui madhara yake? Ni kama ambavyo Rashid Makwilo ‘Chidi Beenz’ alivyo na taarifa zote muhimu kuhusu sumu iliyomo kwenye mihadarati lakini hivi karibuni alikamatwa nayo Air Port.
Chidi alitangaza sana mwaka juzi kwamba ameachana na matumizi ya madawa ya kulevya. Binafsi niliamini kwa namna alivyokuwa anazungumza kwenye vyombo vya habari. Hata hivyo muonekano wake ulikuwa unatia shaka kidogo kuamini kama kweli kaacha.
Namfahamu Chidi, ni mwanamuziki wa Hip Hop aliyekamilika sana. Sauti yake pekee ni mtaji, kwani anaweza kupanda, kushuka na kuigeuza alivyotaka, vilevile anayo staili inayomfanya awe wa kipekee. Ni mkali wa miondoko (swagger) ambayo inampa thamani ya kuwa mwana-Hip Hop mwenye mvuto.
Chidi ana pumzi na nguvu (energy) akiwa jukwaani. Kwa tathmini yangu kama mwandishi wa habari, vilevile mdau katika soko la muziki (hasa kizazi kipya) na sekta ya burudani Tanzania kwa jumla, nathubutu kusema ndiye mwanamuziki wa Hip Hop ambaye hutumia nguvu nyingi jukwaani na kumudu kufanya shoo kwa muda mrefu tena kwa ufanisi.
Mara kadhaa niliwahi kujiuliza, kama alikuwa anaonesha uwezo huo jukwaani ilhali anatumia ‘madude’, je, angekuwa hatumii? Bila shaka angeweza kufanya zaidi. Jicho langu kimuziki linaniaminisha kuwa Chidi alizaliwa ili awe mwanamuziki wa Hip Hop. Ni mkali siyo siri!
Ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wa Hip Hop nchini wenye uwezo wa kutumbuiza kwa ‘live band’ na kukonga nyoyo za hadhira kwa kiwango cha juu. Kama wewe ni shabiki wa Hip Hop, unataka nini kingine pale Chidi anapokuwa jukwaani kifua wazi?
Nimeshafanya kazi nyingi na Chidi, pamoja na sifa yake inayojulikana kwa wengi kwamba ni rapa mkorofi ambaye mara kwa mara hukwaruzana na wasanii wenzake na watu wengine lakini upande ninaoutambua ni kuwa mwanamuziki huyo si kigeugeu kwenye kazi.
Ni mtata sana, hilo hata yeye mwenyewe anajijua. Kujisema kwa watu kuwa ni mkorofi haoni tabu. Siku moja, sikumbuki tarehe ila ilikuwa mwaka juzi, nilipokuwa namtuliza asimvae mtangazaji wa EATV, Allan Lucky, aliniambia yeye ni “arnimal”, akimaanisha mnyama mkali aliye tayari kurarua mtu muda wowote.
Pamoja na sifa zote lakini hata mara moja sikuwahi kukubaliana naye halafu akaenda kinyume na makubaliano. Wakati wa mazungumzo kutofautiana lazima, ila makubaliano yakishafikiwa atatenda kama ambavyo tuliafikiana.
Ni tofauti na wasanii wengi tu ambao hawatumii ‘madude’ lakini si waaminifu katika makubaliano hata kama yapo kwa maandishi. Chidi akiwa jukwaani, anajua afanye nini kwa wakati gani kwa kuangalia sura ya hadhira ambayo anacheza nayo.
Mtazame Ray C, alilishika soko la Bongo Flava siyo Tanzania tu, Afrika Mashariki kwa jumla. Wakati huo dada yetu huyo alitambulika zaidi kwa jina la ‘Kiuno Bila Mfupa’ kutokana na uhodari wake wa kuzungusha nyonga yake, japo kizembezembe, maana huwezi kufananisha na vya wakata nyonga wa siku hizi kama Snura na Shilole.
Wakati Ray C akiwa amelegea kwa matumizi ya madawa ya kulevya, nilizungumza na mdau mkubwa wa muziki Kenya, Refigah anayemiliki lebo ya Grandpa Records, akanieleza masikitiko yake kisha akaniambia: “Pamoja na hali aliyonayo, Ray C akiwa Kenya ni biashara kubwa, Wakenya wanampenda sana, pesa zake zipo njenje.”
Mwanamuziki lulu barani Afrika, Brenda Fassie, alifariki dunia dunia mwaka 2004. Ripoti za kifo chake zipo wazi kwamba kilichomsababishia mauti ni mdawa ya kulevya, kwani asubuhi ya siku yake ya mwisho, alitumia kiwango kikubwa cha Cocaine.
Laiti kama Ray C angechukua kifo cha Brenda kama shule kwake, sina shaka kwamba pengine angekaa mbali na mihadarati. Tatizo ni kwamba akili ya binadamu hufanya kazi tofauti, mara nyingi hushawishika kufanya yanayokatazwa. Reverse psychology ndiyo sababu ya Hawa kumshawishi Adam kula tunda la mti wa katikati kwenye Bustani ya Eden.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, mkongwe wa Hip Hop Tanzania, Terry Msiagi ‘Fanani’ wa Kundi la HBC, alishaanza kulalamika kwamba matumizi ya madawa ya kulevya yamempotezea dira na anatamani kuacha. Yaani kadiri watu wanavyolalamika, ndivyo na wengine wanavyoshawishika kutumia.
Mkongwe Mack 2B Simba hatunaye, kifo chake kilifuata baada ya afya yake kuzorota kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya. Mateso ya Banza Marble na hata kifo cha Ngwair ni mifano hai, sasa ni kwa nini bado zipo taarifa kwamba akina TID wanatumia unga?
Ulimwengu umeshapoteza vipaji vingi kupitia madawa ya kulevya. Kuna ambao walikuwa wanatengeneza fedha nyingi kwa vipaji vyao kama Amy Winehouse, Whitney Houston, Heath Ledger, Cory Monteith na wengineo, leo hawapo nasi. Unga uliharakisha vifo vyao.
Kuna mastaa kama Lindsay Lohan, Robert Downey Jr, Charlie Sheen, Chris Brown, Bobby Brown, Britney Spears na wengineo wengi, wamegeuka mateja. Maisha yao yanavyoharibika si kificho lakini hawajifunzi. Vipaji vinapotea, nafasi yao ya kutengeneza pesa inakuwa finyu. Mashabiki hawapendi mateja.
Ukitaka kuthibitisha hilo ni kuwa mwanamuziki hata awe anapendwa vipi, akisharipotiwa kutumia madawa ya kulevya, hupoteza chati yake haraka sana. Ndiyo maana leo hii ni kazi sana kuwarudisha sokoni wale ambao jamii iliwatema kwa sababu ya uteja. Watafanya muziki mzuri lakini mapokeo si kama zamani.
Wakati muziki wa Tanzania ulikuwa huongei kitu mbele ya Q Chiller, ikabainika kuwa mwanamuziki huyo anatumia ‘madude’. Hapa ifahamike kuwa unga husababisha ufanisi wa kazi ushuke, kisha jamii humuona mhusika kama mtu wa tofauti, maana mtumia madawa ya kulevya ni mhalifu.
Sishangai mtu anapoibiwa vifaa vya gari lake akimtaja Lord Eyez kwa sababu mwenyewe aliamua kujipa sifa mbaya. Wapo wanamuziki wakongwe wanakaa kimya na wakitoka wanarudi na heshima zao kwa sababu hawakuwahi kujiingiza huko. Hata kama walijaribu, hawakutangazwa.
KWA NINI UNGA NA WASANII?
Nimeshafafanua kuwa wasanii hawajifunzi licha ya kuwepo mifano mingi, sasa kwa nini wanaendelea kujiingiza? Zipo sababu kadhaa ambazo nitazifafanua moja baada ya nyingine kutokana na uchunguzi ambao nimeufanya.
Kwanza; kundi kubwa la wanamauziki wanajiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa sababu ya kuiga. Mtu anaweza kumuona mwenzake anatumia, kwa fikra zake akadhani ana faidi sana, hivyo naye kuamua kujaribu. Wanaojaribu wengi huwa hawaachi, mwisho wanatambulika kama mateja rasmi.
Niliwahi kuzungumza na Msafiri Diouf wa Twanga Pepeta, akaniambia kuwa wakati Aisha Madinda anataka kujiingiza kwenye unga, alimuonya kwa sababu alishaona athari zake lakini mwanadada huyo aliona anabaniwa, kwa hiyo akaanza kubwia.
Pointi ya kuiga, hutokana na kuangalia hata wasanii wa nje. Mathalan, mtu anamuona Chris Brown, kisha anaona kwamba na yeye anaweza ‘kulanduka’. Hajui kama mwenzake ana pesa, kwa hiyo anapata huduma nzuri kama chakula na hata kusafisha damu, wa kwetu akijiingiza tu, miezi miwili tayari ‘alosto’.
Nifafanue kuwa haina maana ukiwa na pesa nyingi ndiyo ruhusa kutumia, la hasha! Namaanisha kuwa akina Chris wanapata huduma ambayo angalau inawafanya wasichoke haraka. Ila kuchoka ni lazima ndiyo maana ukipima muonekano wake kabla na baada utaona tofauti kubwa.
Pili; wapo wanaingia kwenye uteja kwa sababu ya makundi. Unakuwa na rafiki ambaye anatumia lakini hujui, unamgongea sigara, kumbe mwenzake ameichanganya na unga. Ukivuta unalewa, unapata stimu, siku nyingine unaulizia kama ile, mwisho nawe unakuwa mtumiaji.
Niliwahi kumuuliza Maunda Zorro baada na yeye kusikia anatumia, kwanza alinihakikishia kwamba hatumii kabisa, ila akanipa ushuhuda wa rafiki yake mmoja aliwahi kuonja ‘fegi’ ya mwenzake studio ambayo ilikuwa imechanganywa na madude.
Upo mfano wa mwanamuziki Kulwa wa Mapacha Maujanja (alikuwa familia ya Vinega). Yeye kwa kauli yake aliniambia kuwa aliwahi kugongea sigara ya wasanii wenzake (alinitajia majina yao) pale Maisha Club lakini alichokutana nacho kilikuwa tofauti, alilewa na siku iliyofuata aliumwa na kichwa vibaya mpaka kujihisi anataka kurukwa na akili.
Tatu; ipo imani ya wasanii kwamba ukitumia madawa ya kulevya unakuwa wa kileo zaidi na hata sanaa utafanya kwa kiwango cha kimataifa. Mwana Hip Hop anaamini akibwia unga, basi atakuwa kama Snoop Dog, The Game, Lil Wayne na wengineo wa Marekani.
Hivyo basi, mwanamuziki anaamua mpaka kujidunga kwenye mishipa akiamini ndivyo anavyokuza sanaa yake. Matokeo yake badala ya kuwa msanii mkubwa, anageuka kuwa teja wa kutupwa. Usicheze kabisa na madawa ya kulevya.
Nne; msongo wa mawazo ni sababu nyingine. Wapo wasanii soko linawakataa, pengine na majukumu ya kifamilia yanawaandama. Wakitazama kuna wenzao wanatengeneza fedha kwa kasi kubwa kama ambavyo na wao iliwahi kuwa upande wao.
Hali hiyo huwa inawachanganya vichwa wasanii kiasi cha kuamua kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, wakiamini wanatafuta suluhu ya msongo wa mawazo wakati kumbe wanakwenda kujiharibia maisha yao kwa jumla.
Tano; wapo wanaoingia kwa sababu ya tamaa, mfano msanii anakubali kubebeshwa madawa na kusafiri nayo kwenda nje kuuza. Hao wanaitwa mapunda. Matokeo yake wanajiingiza kwenye kutumia wakati mwanzoni walijiapiza kusafirisha tu.
Kuna ambao waliamua kutumia baada ya kuchanganyikiwa kutokana na kudhulumiwa pesa za kusafirisha mzigo, wengine walitamani tu kuonja ili wajue wanachokisafirisha kina ladha gani. Ila yote kwa yote, mwisho ni uteja.
USHAURI
Wasanii wetu wanaweza kuepukana na matumizi ya madawa ya kulevya kama tu watazingatia kazi zao na kujiweka mbali na mambo hayo ambayo nimeyataja kuwa sababu ya wengi kujiingiza kwenye uteja.
Muhimu ni kuzingatia kwamba kazi yao ina thamani kubwa, kwa hiyo wailinde. Na watambue kuwa kuharibika kwao, husababisha maumivu kwa mashabiki wao, maana kazi zao huingia ndani ya mioyo ya mashabiki ambao wakisikia habari zao mbaya, huumia sana na kuvunjika mioyo.
By Luqman Maloto