Ulikosa Habari kubwa za ITV, ziko hapa. Ipo taarifa ya Escrow, ajali ya basi iliyoua na Mahakama ya watoto
Walichokisema Wananchi kuhusu ishu ya Ripoti ya Escrow
Baada ya Ripoti ya PAC kusomwa Bungeni na Bunge kuanza kuijadili Ripoti
hiyo watu mbalimbali wameonekana kusikitishwa na jinsi hali ilivyo
ambapo mpaka baadhi ya viongozi wa kidini wametajwa kuhusika katika mgao
wa pesa zilizochotwa kutoka kwenye akaunti ya Escrow.
Mmoja kati ya wananchi hao amesema; “…
Sijui ni Mungu gani ambaye wao wanamuabudu, yaani kama wangepata nafasi
japo ya dakika moja kuchungulia wananchi tunapata shida kiasi gani
wasingefanya mambo wanayoyafanya. Nimesikia kwamba kuna viongozi wa dini
wanaohusika kwenye suala kama hilo, nimesikia Mheshimiwa wetu Waziri
Mkuu alikuwa anajua ishu nzima na hajawahi kuongea jambo lolote mpaka
watu wamekuja kujua yeye ndio anaongea… nimejisikia vibaya na sijapenda…”
Ajali ya basi la Tanga
Siku ya jana Novemba 27 imeripotiwa ajali mbaya ya barabarani ambapo
gari aina ya Coaster iliyokuwa imepakia abiria ilipata ajali kwa
kugongana na lori la mizigo eneo la Mkanyageni Tanga, ambapo watu 11
walifariki kutokana na ajali hiyo na wengine majeruhi ni 25 ambapo
chanzo cha ajali hiyo kimesemekana kuwa ni dereva lori kuyumba na
kuigonga gari hiyo ya abiria.
UNICEF kujenga Mahakama ya watoto Mbeya
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto Duniani UNICEF
limeahidi kusaidia ujenzi wa Mahakama ya watoto Mbeya kutokana na Mkoa
huo kukidhi viwango vya uanzishwaji wa Mahakama hiyo ambapo hii itakuwa
ni Mahakama ya pili kwa Tanzania, nyingine ikiwa ni Mahakama ya Kisutu
Dar.
Mkoa huo umechaguliwa kutokana na kukidhi vigezo vya kuanzishwa Mahakama
hiyo ambavyo ni pamoja na uwepo wa madawati ya jinsia na watoto katika
vituo vya Polisi na pia uwepo wa Waendesha mashtaka na Mawakili wa
Serikali wanaoshughulikia mashtaka ya watoto.