Aliyeongoza msafara kwenda kwa Lowasa asimamishwa kazi



Kamanda  wa UVCCM wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail (Mwakabwanga) (kulia)

KAMANDA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahim Ismail (Mwakabwanga), ambaye aliongoza msafara wa vijana wa Bodaboda kwenda mkoani Dodoma kumshawishi Edward Lowassa kuwania urais, amesimamishwa kazi ya ukamanda.

Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbarali, Brown Hebron Mwangomale, alithibitisha kumsimamisha kazi kamanda huyo kwa kile alichosema kuwa ni kutokana na kukiuka kanuni za jumuiya hiyo.

Alisema kamanda huyo tangu apendekezwe na hatimaye kuteuliwa baada ya kupita katika vikao halali vya Jumuiya hiyo ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa, amekuwa akifanya mambo mengi jimboni humo bila kushirikisha ofisi.
“Ni kweli tumemsimamisha kamanda na baadhi ya vijana kwa siku tisini ambapo pia walikaidi kuja kuhojiwa na kamati tekelezaji ya UVCCM wilaya” 
alisema Mwangomale.

Kamanda Mwakabwanga ambaye pia anatajwa kuwa ni mmoja kati ya makada wa CCM wilayani humo wanaotarajia kutangaza nia ya Ubunge huku taswira ikiwa ni yeye mwenye nguvu na mwekezaji aliyetajwa kwa jina la Haruni, alikiri kupata taarifa za kusimamishwa nafasi ya ukamanda.
“Mimi nipo hapa Mbarali, nimepata taarifa kuwa kuna barua yangu naletewa ambayo inahusu kusimamishwa ukamanda! Awali nilipata barua ya kutakiwa kuhojiwa na kamati ya utekelezaji ambayo haikutaja hata tuhuma zangu, tarehe hiyo hiyo ya kuhojiwa napewa barua ya kusimamishwa! Lakini natarajia kuijibu kwa maandishi” 
alisema Mwakabwanga.

Alisema maamuzi ya namna hiyo ni moja kati ya mambo ambayo yanawakimbiza baadhi ya vijana ndani ya CCM ambapo yeye amesikia taarifa kuwa anatuhumiwa kuwa nyuma ya baadhi ya vijana ambao wanaotaka kiitishwe kikao halali cha kikanuni ambacho ni Baraza la vijana la wilaya.

Mbali na Mwakabwanga, imeelezwa kuwa vijana kadhaa ambao wanaonekana kumuunga mkono kiongozi huyo katika safari yake ya matumaini ya Ubunge, nao wamesimamishwa akiwemo Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya mkoa wa Mbeya, Simon Nyota, ambaye kikanuni anao uwezo wa kuijadili barua hiyo na kumjadili katibu wa wilaya.

Nyota alipotafutwa alikiri kupata barua ya kusimamishwa na akasema “Hizi ni vurugu, Kamati iliyotusimamisha tuliipa siku 90 za kutoa taarifa za umoja wa vijana na kuitisha baraza, lakini leo nashangaa wanataka kutuziba midomo huku Katibu akisema kuwa mimi nilikosea kusimamisha msafara wa Katibu wa mkoa ambaye ni mjumbe mwenzangu katika kikao cha mkoa” alisema Nyota.

Wengine waliosimamishwa kujihusisha na shughuli za umoja wa vijana wa CCM wilayani humo ni pamoja na Elia Bange, Veronica, Alfan Melele na Michael Makao ambaye ni mwenyekiti Rujewa na mjumbe halmashauri ya CCM wilaya ya Mbarali.

“Nimepata barua ya Mei 18, mwaka huu ya kunisimamisha kwa siku 90 kutoshughulika na kazi za umoja wa vijana ambayo inaeleza kuwa nina makosa ya kuvuruga jumuiya, kukataa kuhojiwa na vikao halali, kupuuza maagizo ya ofisi na kuendekeza makundi” 
alisema Makao.

Alisema hali hiyo imekuja baada ya kikao cha baraza la dharula lililoketi Desemba 29,2014 wilayani humo ambalo lilishinikizwa na baadhi ya vijana kuutaka uongozi wa jumuiya hiyo kuitisha vikao vya kikanuni ambapo baraza hilo liliwapa Katibu na Mwenyekiti wake siku 90 za kutekeleza maagizo ya baraza ambapo badala ya kutekeleza, wameamua kuwaziba midomo baadhi ya wanaoonekana wana ushawishi katika kuwabana viongozi hao.

chanzo www.wavuti.com

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …