Mwigizaji maarufu enzi za RTD, Bi Nyakomba aaga dunia
Bi Nyakomba ameaga dunia.
Marehemu Bi Nyakomba alipata umaarufu katika michezo ya maigizo redionio
wakati huo ikirushwa na Redio Tanzania (RTD) akishirikiana na wasanii
wenzake wakiwemo Hamisi Tajiri al maaruf Meneja, Ibrahim Raha al maaruf
Mzee Jongo, Bakari Mbelemba al maaruf Mzee Jangala, Mzee Kagunga, Mzee
Majengo na wengine, amefariki katika hospitali ya Jeshi la Polisi katika
barabara ya Kilaw, alikopelekwa usiku wa kuamkia jana baada ya
kuzidiwa.
Bi Nyakomba alikuwa akiugua kisukari tangu mwaka 2012.
Mwili wa marehemu Nyakomba unatarajiwa kuzikwa kesho saa tisa alasiri
kwenye makaburi ya Chang'ombe jijini Dar es Salaam mara baada ya ibada
ya mazishi itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maurus,
Kurasini.
Ndugu wa familia ya marehemu wamesema Bi Nyakomba amefariki akiwa na
umri wa miaka 64 akiacha watoto sita na wajukuu kumi na watatu.
Enzi za uhai wake, Channel TEN iliwahi kufika katika nyumba yake huko
Keko Juu katika Kata ya Mburahati, Manispaa ya Temeke ili kumjulia hali
wakati akiugua ambapo pamoja na mambo mengine, alihusia wasanii hususan
vijana kote nchini, kuifanya sanaa kaw nidhamu kwa kuwa ni kazi rasmi
kama nyinginezo.
Mwenyezi Mungu alitoa na ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Apumzike pema marehemu Bi Nyakomba.
Pole kwa nyote mlioguswa na msiba huu.