Sitta atangaza nia ya urais ‘kiaina’

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta 
Dodoma/Dar. Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema kati ya waliojitokeza na wanaotajwa kuwania urais, hakuna ambaye anaweza kupambana na kuikataa rushwa na kwamba muda ukifika ataweka hadharani nia yake.
Sitta, ambaye pia anatajwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, alisema si ajabu na yeye kushawishika kujiunga na watangaza nia hao.
“Nikitazama hizi orodha zinazotajwa, sioni mtu anayepambana hasa na suala hili (la ufisadi). Nataka tuongeze nguvu ya wazalendo kupambana na ufisadi na tuwe wa vyama vyote,” alisema spika huyo wa Bunge la 10
Akizungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge baada ya kuulizwa ni lini atatangaza nia ya kugombea urais, Sitta alisema: “Ni namna ya kuangalia mambo tu, bado kidogo maana muda upo mpaka Julai. Nyinyi (waandishi) subirini tu nitawaarifu.”
Wasira, Mwigulu leo
Mchakamchaka wa kutangaza nia unaendelea leo, kesho na keshokutwa kwa wagombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)kutangaza rasmi sababu zinazowasukuma kutaka kuingia Ikulu.
Wagombea hao ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Steven Wasira ambaye leo atakuwa Mwanza kutangaza nia hiyo katika tukio ambalo litarushwa moja kwa moja na vituo viwili vya televisheni.
Pia mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba anatarajiwa kutangaza nia yake kwenye viwanja vya Chuo cha Mipango mkoani Dodoma.
Kesho Profesa Mark Mwandosya atakuwa kwenye ukumbi wa CCM, mkoani Mbeya kutangaza nia yake ya kugombea urais kwa mara ya pili baada ya kushika nafasi ya tatu mwaka 2005. Waziri huyo wa Nchi Ofisi ya Rais atahutubia wakazi wa Mbeya kwenye ukumbi huo maarufu mkoani Mbeya.
Pia mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere anatarajiwa kutangaza nia yake ya urais Mwitongo, Butiama.
Vuguvugu hilo litaendelea keshokutwa wakati Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, naye atakapotangaza nia yake mkoani Mwanza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe ambaye juzi aliliaga rasmi Bunge wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, amepanga kutangaza nia yake jimboni Mtama, mkoani Lindi Juni 7.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …