MAAJABU WATOTO KUFIA KWA GWAJIMA
“KWA kweli sisi kwetu kama kanisa ni maajabu na mshtuko. Inapotokea ajali kama hii bila kutarajia lazima kutokee mshtuko. Hakuna anayependa kutokea kwa hali hii, tumuombe Mungu. Najua mengi yatasemwa lakini ukweli ni kumuachia Mungu tu,” ndivyo alivyoanza kusema Askofu Yekonia Byabaza ambaye ni Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Askofu Byabaza aliyasema hayo alipozungumza na Gazeti la Uwazi kufuatia vifo vya watoto wawili ndugu wa damu moja, Sarah (10) na Goodluck David Oturo (4) waliokufa kwa kunaswa na umeme wakiwa kwenye ibada katika kanisa hilo, Kawe jijini Dar wiki moja iliyopita.
Askofu huyo alizungumza na Uwazi kwenye ibada maalum ya kuaga miili ya marehemu hao iliyofanyika nyumbani kwa wazazi, Mbezi Juu jijini Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita.
Aliendelea kusema: “Ninachokijua ni kwamba hali hiyo imetokea kwa wote baada ya Goodluck ambaye ni mdogo alipoona dada yake amenaswa na umeme alimfuata na kumgusa huku akilia na kusema; dada… dada…ndipo na yeye akanaswa lakini siyo kwamba kuna jambo. Mungu alipanga kuwa vifo vyao vitatokana na njia hiyo.”
MASWALI YA WANAFUNZI
Katika msiba huo uliowaacha midomo wazi waombolezaji, wanafunzi waliokuwa wakisoma na Sarah walikuwa na maswali kwa muda mrefu:
“Kwa nini iwe familia hiyo tu? Kwa nini iwe Sarah na mdogo wake tu? Mbona kulikuwa na watoto wengi! Halafu tunasikia waya uliomnasa Sarah haukuwa umechubuka, sasa kwa nini anaswe?”
Wanafunzi hao muda mwingi walikuwa wakitokwa machozi kupindukia huku wengine wakiishiwa nguvu.
Mmoja wa wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Samuel alisema kwamba, Sarah alikuwa mpole na alikuwa akipatana na kila mmoja, hakuwa mgomvi na alikuwa ana uwezo mkubwa darasani.
KITAALAM
Mtu mmoja msibani hapo ambaye alijitambulisha kuwa ni fundi umeme, alisema kuwa, kwa umeme wa majumbani, mtu akivaa viatu hata kama atakanyaga waya wenye umeme si rahisi kunaswa na kufa.
“Napata shida sana kama kweli Sarah alikanyaga waya wenye umeme. Mbona alivaa viatu tena viatu vyenyewe havikuwa na chuma, kwa nini anaswe? Haya kwangu ni maajabu hasa ninapoambiwa hata huo waya wenyewe haukuwa umechubuka,” alisema fundi huyo.
MAJIRANI, WAALIMU WAZIMIA
Ili kuonesha kuwa, vifo vya watoto hao viligusa wengi, baadhi ya majirani sambamba na walimu wa marehemu Sarah, jumla yao ikipata tisa, walianguka na kupoteza fahamu wakati wakipita kwenye majeneza kuiaga miili hiyo.
Baba wa marehemu hao(katikati) akiaga miili ya wapendwa wake.
MSEMAJI WA FAMILIAKutokana na hofu na mkanganyiko wa vifo hivyo kutanda, gazeti hili lilizungumza na ndugu wa karibu wa marehemu hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini na kumuuliza juu ya maoni ya familia hiyo ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kwa kweli kwangu haya ni maajabu! Mimi si msemaji mkuu wa familia lakini ninachokijua ni kwamba, marehemu kabla ya vifo vyao walishatuhangaisha sana kwa kuumwa, hasa Goodluck. Na ajabu ni kwamba, kuumwa huko, tulipowapeleka hospitali hawakupata nafuu lakini tulipowapeleka kwa waganga wa kienyeji walipona.
“Kifupi ni kwamba, ukisimuliwa historia ya maisha yao kwa ujumla ilitafsiri vifo. Inatuuma sana! Ajabu ya magonjwa yao, walikuwa wakipelekwa kwa waganga wa kienyeji wanapata nafuu.“Baba yao amehangaika nao mpaka basi hali iliyomfanya mama yao kuamua kuwapeleka katika maombi kwa Askofu Gwajima.”
Msemaji huyo: “Nakumbuka Goodluck akiwa na umri wa miaka miwili, siku moja tukiwa ndani ya nyumba iliibuka harufu ya dawa za kienyeji, ghafla yeye alianza kunyooka huku akipoteza fahamu. Alipelekwa hospitali ikashindikana, akapelekwa kwa waganga wa miti shamba akapata nafuu.”
MWAKA MMOJA BAADAYE
“Baada ya mwaka moja alianza kuumwa tena, akawa anatembea huku akizunguka huku na kule bila kusema na mtu. Alionekana kama yupo kwenye ulimwengu wa pekee. Aliweza kupona kwa mganga.
“Safari ya tatu akawa anatembelea makalio huku Sarah naye akianza kuumwa tumbo na kuwa mpole sana. Tuliamua kuwapeleka hospitali mbalimbali lakini hawakupona, tulipowapeleka kwa mganga wa miti shamba wakapona.
“Ndipo tulipogundua kuwa kuna mchezo mchafu unafanyika na hapo ndipo mama yao akawa anakwenda nao katika maombi. Nafikiri mengi zaidi mkamuulize baba yao.”
WAZAZI WASIMULIA
Baba mzazi wa marehemu hao, David Oturo yeye kwa upande wake alikiri kuumwa kwa watoto hao magonjwa ya ajabu ambapo alipokuwa akiwapeleka hospitali hawakupona bali walipata nafuu walipopewa dawa za kienyeji.“Na mimi nimepatwa na mshtuko kuhusiana na vifo vya watoto wangu.
Nimehangaika nao kwa muda mrefu na nilijua wameshapona, ndiyo maana nilimruhusu mama yao kwenda nao kwenye maombi. Sikutegemea kama mauti yangewakuta wote kwa siku moja kule kanisani. Lakini yote namuachia Mungu,” alisema kwa masikitiko mzazi huyo.
Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa marehemu hao alisema:
“Vifo vya watoto wangu siku hiyo kama niliviona tangu nyumbani. Ajabu ni kwamba, moyo wangu siku hiyo ulikuwa na ganzi kwenda kanisani. Lakini nikajipa nguvu tukaenda, kumbe ningeusikiliza moyo nikaacha kwenda, wanangu wasingekufa.
“Lengo la kuwapeleka kwa Askofu Gwajima ni kuombewa ili magonjwa ya ajabuajabu yawatoke, wawe salama nikijua hata kukwepesha vifo vyao maana kusema ule ukweli mimi na mume wangu tulihangaika nao sana, nikajua kwa Gwajima ndiyo nimefika kumbe bado!
MIILI YASAFIRISHWA
Miili ya watoto hao ilisafirishwa Ijumaa iliyopita kwenda Musoma mkoani Mara kwa mazishi yaliyofanyika Jumamosi. Oturo kwa sasa amebaki na mtoto mmoja wa kiume, mkubwa kwa wote.
Uwazi linatoa pole kwa familia ya Oturo kwa msiba mkubwa uliowapata na Mungu awape uvumilivu. Bwana ametoa Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe! Amina.Imeandaliwa