Majambazi wampora bunduki askari, Pwani


IGP Ernesrt Mangu 

Dar/Pwani. Matukio ya uporaji bunduki askari kwa watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, yameanza kujipenyeza katika jiji la Dar es Salaam huku mkoa wa Pwani wakiendelea kuvamia na kuvunja vituo vya polisi.



Katika siku za karibuni, matukio hayo yametokea katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Geita, Tanga na Mtwara ambako uporaji wa silaha ulitokea.


Uporaji ulivyofanyika


Watu 10 wanaosadikiwa ni majambazi wakiwa na mawe na mapanga wamemnyang’anya bunduki aina ya SMG na risasi 30, askari polisi wa Kituo cha Tazara kilichopo eneo la Yombo Station na kutokomea kusikojulikana.



Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara Dar es Salaam, Patrick Byatao alisema Mei 27 mwaka huu saa 1:00 usiku, askari namba H.1574 PC Jineneko, alinyang’anywa SMG yenye namba 56-1402621 na risasi hizo huku majambazi hao wakimshambulia kwa mawe na mapanga.


Byatao alisema kuwa, siku ya tukio askari D.8386 SGT Juma na H.1574 PC Jineneko , walipangiwa kazi lindo la Yombo Station na kila mmoja alikuwa na silaha aina ya SMG na risasi 30.



Alisema askari hao waliacha lindo na kwenda kupata chakula cha jioni, jirani karibu na eneo hilo wakiwa wanakula ulitokea ugomvi kwenye duka la kuuza CD.


“Wakati ugomvi unaendelea ndipo wakaenda kuamulia, walifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili, lakini kabla hawajachukua hatua yeyote walivamiwa na kundi la majambazi hao na kuwapora silaha, huku askari Jineneko walimjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake ambaye amelazwa katika Hospitali ya Temeke na anaendelea vizuri,” alisema Byatao.



Byatao alisema chanzo cha tukio hilo ni uzembe wa askari hao kuacha lindo na kwenda kupata chakula sehemu nyingine.


Alisema jeshi hilo linaendesha msako mkali kwa lengo la kupata silaha na watuhumiwa waliopora silaha hiyo na risasi 30, huku wakiendelea kuwashikilia watu saba kuhusiana na tukio hilo.


“Hata hivyo, hadi sasa , silaha hiyo haijapatikana na jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na raia wema, vituo vya polisi na kikosi vilivyopo jijini humu na nje ya Dar es Salaam,” alisema Byatao.



Alisema wanaendelea na uchunguzi ili kuangalia chanzo cha tukio hilo huku akiwataka wananchi kutoa taarifa polisi kwa watu wanaomiliki silaha, kwani wakikaa kimya inaweza kutumika kuwadhuru, hata maafa.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini