Sugu Akomalia Uhuru wa Habari, Alaani Kitendo cha Kumtishia Maisha Reginald Mengi
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu |
KUMINYWA kwa uhuru wa habari na maslahi duni ya wanahabari ni mjadala ambao umetawala Bunge wakati wa kujadaili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani, msemaji mkuu kwa wizara hiyo, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amesema “taswira nzuri ya Tanzania kimataifa kama nchi inayofuata utawala bora na demokrasia inazidi kupotea kutokana na ubabe wa Serikali ya CCM katika kuminya uhuru wa habari nchini”.
Sugu amesema kushindwa kwa hila za serikali ya CCM mbali na kufungia magazeti na hata kuwateka, kuwatesa na kuwaua wanahabari wanaotimiza wajibu wao sasa kumehamia katika kutunga sheria kandamizi ambazo zina malengo ya kuwafunga midomo wanahabari.
“Ni hivi karibuni, vyombo vya kimataifa ikiwemo gazeti kongwe la Washington Post la Marekani, vilianika ubabe wa serikali ya CCM na kushinikiza wafadhili na wahisani hasa Serikali ya Marekani na Benki ya Dunia kusitisha kuipa Tanzania misaada ili kuishinikiza kuzirekebisha sheria hizo kandamizi ambazo zilisainiwa na Rais Kikwete hivi karibuni kwa kuwa zinaminya uhuru wa habari,”amesema.
Sugu amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mitandao ambayo inalenga kuua uhuru wa habari hata baina ya mtu na mtu ambapo mtu anaweza kwenda jela kwa kosa la kufowadi ujumbe, taarifa ama picha ambayo ameipokea kutoka kwa mtu mwengine.
“Lakini pia, vyombo vya kimataifa vinaeleza kuwa kupitishwa kwa Sheria ya Takwimu kutatia hatiani watu hasa wanahabari kwa kigezo kuwa wametoa takwimu ambazo serikali itaona si za kweli na bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),”amesema.
Amesema inashangaza kuona kuwa Taifa linapelekwa gizani kwa sheria hizi za kibabe zisizozingatia dhana ya uwazi ambayo serikali inajidai kuitekeleza.
Sugu ameongeza “Sote ni mashahidi kuwa mara nyingi serikali imekua haitoi takwimu sahihi za mambo mbalimbali na kwa nyakati tofauti serikali pia imekiri kuwa haina takwimu kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo taarifa za ajira na ukosefu wa ajira.”
Amehoji kuwa, leo hii unapowanyima watu uhuru wa kutoa taarifa zinazoambatana na takwimu za masuala husika mpaka kupata kibali cha Ofisi ya Takwimu, serikali inalenga kuficha ukweli gani?
“Muendelezo wa malalamiko dhidi ya sheria hizo kandamizi pamoja na muswada wa habari ambao unaelezwa kuwa katika mkakati wa kuletwa ndani ya Bunge hili, umepingwa vikali pia na wadau wengi nchini ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT),” amesema.
Kambi pia imelaani taarifa za kutishiwa maisha kwa mmiliki wa kituo cha televisheni cha ITV, Reginald Mengi kwa madai kwamba kituo chake kimekua kikitoa habari za kiuchochezi zinazosababisha kuyumba kwa serikali ya Rais Kikwete ikiwemo ya kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya Escrow.
Hata hivyo, katika kujibu hoja za wabunge Waziri Fenella Mkangara na naibu wake Juma Nkamia, walikanusha taarifa hizo wakisema kama suala hilo lingekuwa na mashiko, Mengi angekwenda kulalamika kwenye vyombo husika.
Kuhusu wadau wa habari na wamiliki kupinga muswada mpya wa habari wakiwemo MOAT, Nkamia amesema serikali itajitahidi kuzingatia maslahi ya waandishi walioajiliwa katika vyombo vya habari vya serikali.
Hata hivyo amewataka wabunge kuunga mkono muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari utakaosomwa bungeni mara ya pili kwamba ndio utasimamia maslahi ya waandishi wa habari.
“Serikali imeleta bungeni muswada wa habari. MOAT wanaupinga. Labda niwambie jambo moja kuwa hawa wanatetea maslahi yao na sio maslahi ya waandishi wa habari,”amesema Nkamia.
Mapema, mbunge wa Viti Maalum, Faida Bakari (CCM), imeitaka serikali kujenga ofsi ya waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam ili kuwaondolea adha wanaporipoti habari za Bunge.
Faida amesema “waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa shida. Hapa mjini Dodoma serikali imewajengea ofisi nzuri. Lakini katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam hakuna ofisi ya waandishi wa habari.
“Wakati wa vikao vya kamati za Bunge pale jijini Dar es Saam waandishi wa habari wanasimama koridoni kuanzia asubuhi hadi jioni, hawana hata sehemu ya kukaa. Serikali iwajengee ofisi kama ilivyofanya hapa Dodoma,” ameeleza.
Aidha, imeitaka serikali kuzingatia maslahi ya waandishi wa habari na ihakikishe wanakuwa na sare za Taifa za kufanyia kazi zao hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu ili waweze kutambulika.
Faida pai ameitaka serikali kuweka utaratibu mzuri ambao utawabana waajiri kuwawezesha wanahabari kupata mikopo ya vyombo vya usafiri kama magari au pikipiki ili kuwarahisishia utendaji kazi.