Mabomu ya machozi yarindima Mwanza


Polisi mkoani Mwanza wametumia mabomu ya machozi mapema leo kutawanya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema walioingia mitaani kushangilia wakiamini wagombea wao wanaongoza katika matokeo ya awali. 


Tukio hilo limetokea kwenye kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Mlimani, eneo la Butimba, Ghana na Shule ya Msingi Buzuluga kwenye majimbo ya Nyamagana na Ilemela. 


Taarifa toka jijini humo zinasema kundi la watu waliokuwa vituoni wakisubiri kubandikwa kwa matokeo hayo, lililipuka kwa shangwe, nderemo na shamrashamra baada ya matokeo hayo kubandikwa na wasimamizi wa uchaguzi wakiamini wagombea wao wanaongoza. 


Mwandishi wetu aliyeko jijini Mwanza amesema polisi waliingilia kati na kufyatua mabomu ya machozi kutawanya wafuasi hao. 


Katika uchaguzi wa mwaka huu, mgombea ubunge wa Chadema na mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Nyamagana, Ezekiel Wenje anachuana vikali na aliyekuwa Meya wa jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula wa CCM.


Katika jimbo la Ilemela, mbunge anayemaliza muda wake, Highness Kiwia wa Chadema anatetea nafasi yake kwa kupambana na mgombea wa CCM, Anjela Mabula. 


Uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani umefanyika jana Oktoba 25, mwaka huu ambapo takribani Watanzania milioni 22.7 wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu kwa upande wa Tanzania Bara huku kwa upande wa Zanzibar zaidi ya wapigakura laki tano wamejiandikisha.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini