UKWELI Kuhusu ROSE MUHANDO!

BWANA Yesu asifiwe dada yangu Rose Muhando. Habari ya uzima. Vipi unaendeleaje na kazi ya kumtukuza Mungu? Bila shaka Mungu ni mwema, bado anakupigania pamoja na magumu yote unayopitia.

Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu maisha yanasogea na bado anaendelea kunijalia, namshukuru kila wakati.

Nimekukumbuka leo kwa barua. Nimeguswa na mambo tofauti ambayo yanaripotiwa kuhusu wewe. Kwanza niwe mkweli, nimeshawishika kukuandikia kwa sababu nauona mchango mkubwa ulioutoa tangu ulipobarikiwa kuanza kuonesha karama ya uimbaji.

Wapo watu wameokoka kwa ajili yako. Wapo watu uimbaji wako umekuwa faraja katika maisha yao. Wapo ambao walikata tamaa ya kuishi lakini kupitia nyimbo zako, waliinuka na kuanza upya safari na sasa wanaishi katika mwanga mpya.

Kwangu mimi hiyo ni zaidi ya kuimba. Ni zaidi ya kueneza Neno la Mungu. Wewe nakuona kama mtu pekee sana ambaye unapaswa kuishi tofauti na watu wa kawaida. Kama unawabadilisha watu, kama unaokoa, utashindwaje kujiokoa mwenyewe?
Mara kadhaa umeandikwa kuhusu mambo mabaya, lakini lengo langu ni moja tu; kutaka kukueleza kwamba una nafasi ya kujisahihisha na kusonga mbele. Hakuna haja ya kuangalia watu wanasema nini juu yako, usitafute mchawi, badilika na anza ukurasa mpya.

Najua katika mambo ambayo umekuwa ukituhumiwa nayo hususan yale ya kulipwa fedha na kutotokea kwenye matamasha, kuna ambayo yana ukweli na mengine ni uzushi. Yawezekana wenye chuki binafsi, hawapendi kuona unaendelea kuhubiri Neno la Mungu, usiwape nafasi ya ushindi.

Hao wanasubiri kuona unaangamia. Wanataka kuona hausikiki. Wanataka kuona unateseka. Wanachukia mafanikio yako. Tena wengine wanachukia bila hata kuwa na sababu ya msingi. Mungu ni mwaminifu, atakupigania katika hilo.

Usiwachukie watu wa aina hiyo ila tengeneza njia zako vizuri ili wakose la kusema. Kama walikuzushia kuhusu malipo ya shoo, epuka kuingia mikataba ambayo unaona itakuletea shaka mbele ya safari. Waepuke watu ambao wanakuzunguka halafu wakienda pembeni wanakusema.

Fanya kazi yako kwa bidii, muombe Mungu azidi kukupa maarifa, busara na hekima zaidi ya kuishi na watu. Kama kuna mahali unaona kweli ulifanya kosa, ulitenda dhambi, tubu na umrudie Mungu wako kwani Mungu wetu ni mwaminifu na anasamehe saba mara sabini.

Hujatenda kubwa ambalo haliwezi kusameheka. Mazuri yako ni mengi tu hapa duniani, rekebisha hayo niliyokwambia hapo juu, naamini utaanza upya maisha mapya ya kiroho.
Bila shaka utakuwa umenielewa dada’ngu, Mungu akubariki sana. Nakutakia mafaniko mema na uzidi kuhubiri Injili kupitia uimbaji.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini