RAIS Mteule Dr John Pombe Joseph MAGUFULI Full Kicheko!

RAIS Mteule John Pombe Joseph Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa ni full kicheko kufuatia kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais 2015. 
Katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam jana, mbele ya wawakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo, waandishi wa habari wa ndani na nje, waangalizi wa uchaguzi kutoka jumuia za kimataifa na waalikwa wengine, Jaji Lubuva alisema Magufuli, ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi, alipata ushindi wa asilimia 58, akimshinda mpinzani wake wa karibu, Edward Ngoyai Lowassa wa Chadema, aliyemfuatia kwa kupata kura asilimia 39.

Ushindi wa Dk. Magufuli dhidi ya Lowassa ambaye amelalamika kuchezewa rafu, ulianza kuonesha dalili tangu kuanza kutangazwa kwa matokeo hayo Jumatatu iliyopita, kwani mara zote alikuwa mbele ya mpinzani wake huyo wa karibu.

Mara baada ya kutangazwa ushindi huo, wafuasi wa CCM katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake walilipuka kwa furaha, wakipongezana kwa kazi kubwa na ngumu waliyoifanya ndani ya miezi miwili ya kampeni, ambazo kwa mara ya kwanza walikumbana na upinzani mkubwa kuliko chaguzi zote zilizopita.
“Dah, afadhali jamani amepita Magufuli, tunaamini huyu mtu ataendeleza makali yake kama alivyokuwa waziri, tunategemea alete mabadiliko makubwa kwa utendaji wa watumishi wa serikali, mafisadi sasa mwisho wao umefika,” alisema mama mmoja mkereketwa wa CCM, aliyejitambulisha kama Mama Tabu, aliyekutwa katika eneo la Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam akiwa anacheza mdundiko na wenzake

KUMBE JANA ILIKUWA BETHIDEI YAKE
Katika hali ya kustaajabisha, jana ilikuwa ni siku ya matukio mawili makubwa maishani mwake, kwanza ikiwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa rais huyo mteule, ambaye pia alizaliwa siku kama ya jana, Alhamisi, miaka 56 iliyopita na kutangazwa kuwa kiongozi wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

“Kuna watu wengine wana bahati zao hapa duniani, yaani mtu leo ni kumbukumbu ya siku yako ya kuzaliwa, halafu unapewa zawadi ya kutangazwa kuwa rais wa nchi, kwa kweli ni jambo kubwa sana, ingawa jukumu alilopewa ni zito, tuna imani atalimudu,” alisema kijana mwingine aliyesema ni mfuasi wa upinzani lakini aliyempigia kura ya urais Magufuli.

MASTAA WAMFUNGUKIA
Mastaa mbalimbali wa muziki na filamu waliokuwa katika timu mbalimbali za kampeni za mgombea huyo wa CCM, walisema waliutarajia ushindi wake, hasa kwa jinsi walivyozunguka nchi nzima kumnadi na wengi kuonekana kumkubali kulingana na historia yake ya utendaji. Unataka kusikia walichokisema kuhusu ushindi wa Magufuli? Nenda ukurasa wa 9.

KUTOKA KWA MHARIRI
Tunachukua nafasi hii kumpongeza Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na tunamtakia kila la kheri katika kutimiza majukumu yake.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …