Barua ya Wazi kwa Rais Wetu Dk. John Pombe MAGUFULI

magufuli_aapa

Rais John Pombe Magufuli.

TUNACHUKUA fursa hii ya kipekee kukupongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa fursa aliyokupa Mwenyezi Mungu kuongoza taifa hili la Tanzania.

Tunapenda kukueleza mambo ambayo sisi wadau wa afya tunayaona hayaendi vyema na yanatakiwa kurekebishwa haraka. Kuna mpango unaofanywa chinichini wa kuipora kazi Ofisi ya Taifa ya Madawa (Bohari Kuu ya Madawa) kuhusu suala la kununua, kuhifadhi na kusambaza shughuli za utoaji chanjo kwa mikoa na wilaya zote nchini, jambo ambalo linafanyika kisiasa zaidi na limebeba maslahi ya watu binafsi.

Mheshimiwa Rais, zipo sababu nyingi za msingi kwa nini Bohari Kuu ya Madawa inapaswa iendelee kufanya kazi hii.
Hii ni kutokana na kuwa na utaalamu wa kutosha juu ya kazi hii, kuwa na uzoefu wa miaka mingi, kuwa na miundombinu inayojitosheleza katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma stahiki kwa wakati na inaaminika kwa kutoa huduma husika.

Hofu yetu ni kwamba, iwapo Bohari Kuu itanyang’anywa kazi hii, kiwango cha utoaji huduma kitashuka na kusababisha huduma kutolewa chini ya kiwango na kusababisha madhara kwa shughuli ya utoaji chanjo chini, na hivyo kusababisha vifo vingi vya watoto ikiwa ni pamoja na kushindwa kufikia lengo la kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Hilo litasababisha nchi yetu kuwa nje ya lengo la kimataifa la kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri huo.

Hali hiyo itakuwa imekwamisha pia agizo lako la kila mtu kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ofisi anayotolea huduma kwa umma, maana hiyo ndiyo serikali yake iliyoko madarakani.

Mheshimiwa Rais, tatizo jingine ni uwepo wa madaktari wengi kwenye miradi inayoendeshwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bila kuzingatia kuwa wanapaswa kutoa huduma zaidi kwenye hospitali mbalimbali na wala si kuwepo kwenye miradi ambayo inaweza kutekelezwa na watumishi wa kada zingine.

Tunasema hivyo kutokana na umuihimu wa madaktari na kulinganisha na kazi wanazofanya katika miradi hiyo. Hatusemi miradi hiyo isiwe na madaktari kabisa, la hasha! Mathalani, utakuta mradi mmoja una madaktari sita hadi kumi wakati kwenye mradi huo hakuna wagonjwa! Je, ni hospitali ngapi nchini zina uhaba wa madaktari?
Tunachotaka ni vipawa walivyovipata watu kutokana na kodi za Watanzania, vitumike vyema na mahali sahihi.

Mheshimiwa Rais, tumeyaleta yote hayo kwako si kwa kumchongea mtu yeyote, bali kutekeleza msemo wenye mantiki uliokuingiza madarakani wa ‘HAPA NI KAZI TU!’ Tunakuhakikishia Mheshimiwa kwamba sisi tupo nyuma yako katika kutekeleza yote utakayotutuma.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu akupe hekima na maisha marefu zaidi ukiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika!

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini