Wabunge Mtegoni: Rais MAGUFULI Aombwa Kufuta Posho za Zisizo na Umuhimu

RAIS John Magufuli ametakiwa kufuta posho zote zisizokuwa za lazima kwa wabunge huku watunga sheria hao wakitakiwa kueleza waziwazi msimamo wao kuhusu kukataa posho hizo ili fedha zitakazookolewa zitumike kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika majimbo yao.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo, Ally Hapi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Dk John Magufuli katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini.

Hadi sasa wabunge ambao wamekataa kupokea posho ya vikao vya Bunge ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto ambaye akiwa katika Bunge la 10 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitangaza kutochukua posho akitaka zielekezwe kwa wapiga kura wake.

Mwingine ni Mbunge mpya wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) aliyeandika barua kwa Katibu wa Bunge huku akitoa msimamo wake kwamba hataki posho hizo, badala yake zielekezwe jimboni kwake kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili wapiga kura wake.

Jana, katika akaunti yake ya Twitter, Zitto aliandika kuwa, “Mshahara wa mbunge ni 3.8m kila mwezi. Posho ya Ubunge 8m kwa mwezi. Posho ya kujikimu (perdiem) 120,000 kwa siku, kukaa 200,000 (posho ya vikao) kwa siku. Fedha za mfuko wa jimbo huwa around 48 mil kulingana na jimbo.

Sasa maposho yote hayo. “Mwambie mbunge wako hizo posho apeleke jimboni kusaidia jamii, hizo ni kodi zetu mimi na wewe. Kuna wabunge Majimbo yao hata matundu ya vyoo vya shule hamna wakati laki moja tu yatosha.”

Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo, alisema wananchi pia wawasimamie wabunge wao waliowachagua katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu ili waeleze msimamo wao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho.

Alisema Jukwaa linatambua Dk Magufuli ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo hivyo wanamuomba kufuta kabisa posho kadhaa kwa wabunge.

“Tunamuomba Rais kufuta posho zote zisizokuwa za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma,” alisema. Aliongeza kuwa wabunge wote bila kujali vyama vyao waungane na Kingu pamoja na Zitto katika kukataa malipo ya posho ili kupunguza mzigo mkubwa ambao serikali inaubeba kuhudumia wabunge.

Kuhusu msimamo kwa wabunge, alisema mbali ya kuwepo kwa wabunge wachache waliokataa kupokea fedha hizo ni wakati sasa kwa wabunge wengine kueleza msimamo wao juu ya suala hilo.
“Jana (juzi), Mbunge wa Singida Magharibi, Kingu aliandika barua kwa Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge katika kipindi chote cha miaka mitano kuanzia 2015- 2020,” alisema Hapi.

Alisema mbunge huyo anakuwa wa pili baada ya Zitto kutoka hadharani katika Bunge la 10 na kukataa posho hizo ambazo msingi wake alidai ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi.

Alisema Jukwaa hilo linapongeza maamuzi ya Kingu na Zitto kwa ujasiri wake na uzalendo wake kwa taifa ikiwa ni kuuunga mkono juhudi za Rais kwa vitendo wakitambua kuwa ubunge ni utumishi na wala sio utukufu na kazi hiyo ni ya kuwawakilisha wananchi na sio kuwanyonya.

“Jukwaa linatambua mapambano hayo yaliyoanzishwa na Kingu yanahitaji kuungwa mkono na Watanzania wote wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama,” alisema Hapi na kuongeza kuwa baada ya msimamo wa Kingu, wapo wabunge wasiokuwa na huruma hawakufurahishwa na hatua hiyo na wengine kuanza kumpigia simu na kumtumia ujumbe mbalimbali.

Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa hilo, Mtela Mwampamba alisema wataongoza vuguvugu lenye kuwaelimisha wananchi pamoja na kufanya maandamano ili wabunge watoe msimamo wao ili kumuunga mkono Rais Magufuli katika uamuzi aliochukua wa kubana matumizi ya serikali. 

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini