MAPYA Kuhusu Hukumu ya Mazishi ya Mwenyekiti wa Chadema Geita, Alphonce MAWAZO
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kesho mchana inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na ndugu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo wakipinga zuio la polisi kuchukua na kuaga mwili wa Mawazo kwa maelezo ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu.
Baba mdogo wa Mawazo, Mchungaji Charles Rugiko alifungua kesi hiyo juzi kutokana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo kupiga marufuku shughuli za kuaga mwili wa marehemu aliyeuawa na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM Novemba 14.
Usikilizaji wa kesi hiyo uliochukua saa tatu kutokana na uwapo wa mvutano wa kisheria kwa mawakili wa pande mbili, ilianza kusikilizwa saa 5:00 asubuhi hadi saba adhuhuri na Jaji Lameck Mlacha.
Kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2015, iliyovuta hisia za watu wengi jijini Mwanza, mlalamikaji anaomba mahakama kuondoa zuio la Polisi kuzuia kuagwa mwili wa Mawazo; Kutoa tamko la zuio la RPC kuwa ni batili na kinyume cha sheria na mahakama imkataze Kamanda Mkumbo kujihusisha na shughuli za mazishi na kuaga mwili huo.