MJOMBA MRISHO MPOTO: Mtu wa Darasa la 7, Mafanikio Lukuki...Afunguka SIRI ya Kufanikiwa Kwake!

MPENZI msomaji wa simulizi hii nzuri, tamu na ya kusisimua wiki iliyopita tuliishia pale Mrisho alipoweka wazi makampuni anayoyaongoza na jinsi alivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza ndoto yake ya siku nyingi juu ya kuwapa ajira vijana wengi.
 atika moja ya kampuni yake ambayo ni International Market (IM) alikuwa amewaweka warembo tu kama 19, je nini kiliendelea. Songa nayo mwenyewe…

Katika suala la muziki Mpoto, mashabiki wako wengi wanatamani kukuona unatoka kimataifa, mbona hawaoni hili? Namuuliza kichokozi…
“Ujue hakuna kitu kizuri duniani kama kutengeneza jina lako kwanza na likakubalika kwa kila mmoja, kuna vitu viwili ambavyo watu wengi wanashindwa kufahamu.
“Kuna maudhui na fani, fani ni kitu kinachojenga maudhui ambayo yapo ndani mwangu kwa kila ninachokifanya. Katika maisha yangu kama nilivyowahi kueleza hapo mwanzoni, sikuwahi na wala sikupenda kutegemea vitu vya hovyohovyo.

“Wengi wanatoka kimataifa kwa kulazimisha kiki, wanashindwa kujipanga mwisho wake wanakuwa wa hovyohovyo. Kama nilivyoelezea katika simulizi hii ya kweli ya maisha yangu, niliwahi kutoboa kimataifa na Global to Global Shakespear ya Uingereza ambao huwa wanaandaa matamasha makubwa duniani.

Hongera kwa hilo, labda ufafanue vizuri Mrisho, ipoje hiyo Global to Global Shakespear?
“Ahhhaaa, hii Global to Global Shakespear kama nilivyosema awali huandaa matamasha makubwa ya muziki, filamu na mengine mengi, kipindi cha nyuma walikaa chini na kufanya utafiti ambapo waliungana na Kampuni ya Theatre ya Kenya kutafuta watu gani wanaweza kuwa wahusika katika Filamu ya 1846.

“Nadhani umeona ni kwa namna gani mtu kama mimi niliyetoka elimu ya darasa la saba na kuwa mtu wa kimataifa, umeona ni jinsi gani watu wenye elimu zao lakini hawajawahi kupata fursa kama nilizopata mimi. Sasa hawa Waingereza wa Global Shakespear walinichukua na kunipeleka kwenye matawi yao zaidi ya saba ambayo yapo nchi tofauti duniani kama vile India, Sweden, Norway, Ujerumani, Italia, Ubelgiji na nyingine nyingi.”

Mrisho tuendelee kwenye muziki unaofanya, kwa nini huendani na ushindani wa soko la kimuziki nchini kwa maana ya kutoa wimbo mpya mara kwa mara?
“Kwanza ieleweke kuwa muziki ninaofanya ni muziki wa kumsukuma mtu kimawazo, ninafanya muziki wa inspiration na wala sifanyi muziki wa biashara ndiyo maana hata siku moja huwezi kuniona kwenye majukwaa makubwa ya hapa nchini wala kumbi za starehe nikitoa burudani.

“Tangu nimeanza muziki rasmi, kila mwaka lazima nitoe wimbo mmoja na hadi sasa ukipiga hesabu za haraka nina nyimbo kama kumi na moja. Wimbo wangu wa mara ya mwisho (Njoo Uchukue) nimeutoa mwaka jana hivyo mwaka huu bado sijatoa wimbo, kwa hiyo nina deni kwa mashabiki wangu.

“Tukija katika utungaji bwana mimi niko wa kitofauti sana, huwa natunga pale tu nimepata wazo linalotakiwa liifikie jamii yangu, na hiyo haijalishi hata nikiwa naendesha gari nitahakikisha napaki pembeni kisha naandika mistari kadhaa naendelea na safari ili wazo nisilisahau,” anasema Mrisho.
Itaendelea wiki ijayo.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini