Julius Mtatiro Apinga Kitendo Cha Mkuu Wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda Kuwasweka Rumande Maofisa Ardhi Kwa Masaa 6

Ndugu zangu, muda huu nimeona kwenye mitandao kadhaa watu wakifurahia hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu yetu Paul Makonda kutoa amri (ambayo imetekelezwa) ya kuwaweka ndani wataalam wa ardhi ambao walishindwa kufika eneo la kazi kwa wakati.

Binafsi siungi mkono kitendo cha watendaji kuchelewa maeneo ya kazi lakini zaidi ya yote siungi mkono kitendo cha mkuu wa wilaya kuwaweka ndani watendaji kwa kosa la kuchelewa kazini.

Madhara ya kuwachekea wakuu wa wilaya pale wanapotoa amri zinazokiuka haki za msingi za wafanyakazi ni makubwa mno. Huko nyuma tulizoea mambo haya kufanywa na wakuu wa wilaya enzi za Nyerere, hatutarajii hadi leo wakuu hawa kuendesha wilaya zao kwa amri.

Ni muhimu sana masuala ya kazi yaendeshwe kwa sheria na kanuni za kazi na huyo mtu anayefurahia mamlaka (haramu) ya ma DC kuweka watu ndani atakuwa na matatizo makubwa. Watu wanapaswa kuwekwa ndani kama wamefanya makosa kwa mujibu wa sheria na si kama apendavyo DC.

Tuijenge nchi yetu kimfumo zaidi kuliko ki-amri, nchi zinazoendeshwa kwa amri amri huwa hazifiki kokote, kama tutashindwa kujijenga kimfumo katika miaka hii mitano tukategemea kuendesha nchi kwa amri, matamko na mikwara - ikifika 2020 tutaulizana nini kilifanyika na sote tutabaki kusimulia matamko lukuki yaliyotolewa.

Nimalizie tena kwa kuwakumbusha kuwa "Afrika itajengwa na mifumo imara, watu imara hawawezi kuijenga Afrika maana siku moja watakufa, na kama watakufa bila kuacha mifumo imara - yale yote waliyoyafanya yatapotea haraka ".

Ndugu yetu DC, Paul Makonda, tujengeeni mfumo imara utakaofanya wafanyakazi wote kuwa kazini kwa wakati, (msijijenge ninyi) watu imara na amri lukuki!
 
Mtatiro J.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini