"Hatujaridhia kumuachia Maalim Seif kutangazwa mshindi wa Zanzibar" yasema CCM


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekanusha taarifa iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii ya kuridhia Mgombea wa Chama Cha (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad atangazwe kuwa Rais wa Zanzibar. 


Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kisiwandui mjini hapa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema wamepokea kwa msikitiko makubwa taarifa hizo alizoziita za uzushi. 


Alisema chama chake hakipo tayari kuvunja katiba wala sheria kwa kuridhia kuwa Maalim Seif atangazwe, kwani uchaguzi uliofanyika tayari umefutwa rasmi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupitia Gazeti la Serikali. 


"Mtandao huo wa kijamii ulidai kuwa mimi Naibu Katibu Mkuu niliwataka wananchama na wananchi wote kuridhia hatua hiyo iliyofikiwa ya chama chetu kuridhia kuapishwa Maalim Seif, huku nikisisitiza kwa kuwataka wananchi wote wajitokeze kwa wingi katika sherehe za kuapishwa rais", alisema Vuai. 


Aliongezea kusema, "mbali ya hayo pia tarifa hizo zilinisingizia nimesema kwa kuwataka wananchi waridhie kuwa Dk Ali Mohamed Shein kuwa ni Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar mara bada ya kuapishwa kwa Maalim Seif kuwa Rais". 


Alidai taarifa zote hizo zinaonekana kuwa zimeaandaliwa na kundi maalum lenye kutaka kuivuruga (CCM) na wananchama wake na pia kuvuruga mshikamano. 


Alisema wanatarajia kukutana na wanasheria wa Chama hicho ili kufanya utafiti juu ya waliotoa taarifa hizo na wakigundulika hatua za kisheria zitachukuliwa. Kwa upande wa mazungumzo ya kukwamua hali tete ya kisiasa Visiwani, yanayoendelea kati ya Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif Sharif Hamad, Vuai alisema, wao kama Chama wanayapongeza kwa nguvu zote. 


Alisema kuwa ni matarajio yao kuwa mazungumzo hayo yanaweza kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla huku akisisitiza kuwa mazungumzo hayo hayataweza kuwa mbadala wa sheria. 


Alifafanua kwa kusema kuwa mazungumzo hayo hayataweza kwenda kinyume na sheria ya nchi kwa kuendelea kutangazwa matokeo ya uchaguzi uliofutwa bali inaonekana kuwa yana lengo la kudumisha amani ya nchi kwa viongozi hao. 


Alisema kuwa kwa hivi sasa Chama Chao kinajiandaa kwa nguvu zote katika kushiriki uchaguzi wa marudio na kusema kuwa wako tayari kwa kupiga kura wakati wowote.


"Chama chetu kimo katika harakati za kurejea uchaguzi mara tu Tume itakapoutangaza”,alisema.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini