Picha 37 za ziara ya Mkuu wa wilaya alivyokutana na vyoo vya ajabu ziko hapa


Hiki choo cha ajabu kiko Shinyanga maelezo yapo chini.Leo Jumatatu Novemba 30,2015 ambapo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameanza kufanya ziara kutembelea kata za manispaa hiyo ili kuangalia hali ya usafi wa mazingira kubwa zaidi ni kukagua vyoo vya wananchi ilimkukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.

Mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga alikuwa ameambatana na mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna,mwanasheria wa manispaa hiyo Simon Jilanga,afisa afya wa manispaa hiyo Heri Nakuzelwa,waandishi wa habari na askari wa jeshi la polisi.

Mkuu huyo wa wilaya ametembelea kata ya Chibe na Kambarage na kubaini kuwa kaya nyingi hazina vyoo na kuagiza wajenge vyoo haraka huku akifunga maduka matano kutokana na kukosa vyoo.

Mwandishi,Kadama Malunde alikuwepo kwenye msafara huo ametusogezea picha 37 kilichojiri....


Ziara ilianzia katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Chibe katika manispaa ya Shinyanga.Pichani ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(mwenye kofia) akijiandaa kutembea mtaa kwa mtaa kukagua vyoo.Ziara ya mkuu huyo wa wilaya imekuja siku chache tu baada ya kufanya mkutano mkubwa na akina mama wa manispaa ya Shinyanga kujadili namna ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambapo mpaka sasa umeua watu watatu kati ya wagonjwa 98 waliripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo unaotokana na mtu kula au kunywa kinyesi cha mtu mwingine baada ya kuingia kwenye maji au chakula.


Msafara wa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ukielekea katika mtaa wa Chibe ambapo katika kata ya Chibe ina jumla ya kaya 1500 lakini kaya 398 hazina vyoo,lakini kati ya hizo kaya 1500 nyingi hazina vyoo bora



Mzee Jilili Njinya(kushoto) akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kwanini hana choo katika familia yake na kuahidi kujenga ndani ya siku 7


Hii ni familia katika mtaa wa Chibe katika manispaa ya Shinyanga kulia ni choo cha familia hiyo


Familia ya Shija Kabakuli katika mtaa wa Chibe iliyopewa wiki moja ijenge choo kwani hawana choo na matokeo yake hujisaidia vichakani hali inayochangia kuwepo kwa ugonjwa wa kipindu pindu



Mwananchi akijitetea na kuahidi kujenga choo



Choo katika moja ya familia katika mtaa wa Chibe


Kushoto ni mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna,katikati ni afisa mtendaji wa kata ya Chibe Daniel Mtasibwa na mwandishi wa gazeti la Nipashe wakiwa katika mtaa wa Chibe kuangalia vyoo vya wananchi



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisikiliza maelezo kutoka kwa mtoto baada ya kuulizwa wazazi wake mbona hawaonekani nyumbani.....kumbe walikimbia baada ya kusikia kuna ukaguzi wa vyoo kutokana na familia hiyo kukosa choo na kulazimika kutumia choo cha jirani yao

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoa agizo kwa diwani wa kata ya Chibe John Kisandu juu ya familia ambazo hazina vyoo ambapo alitoa muda wa siku 7 wajenge vyoo na baada ya hapo atarudi kukagua




Waandishi wa habari wakishangaa choo cha aina yake...mchana hakitumiki kwa sababu hakina ukuta wala paa...yaani peupee....giza likiingia mtu anafanya yake


Choo katika familia mtaa wa Chibe kata ya Chibe manispaa ya Shinyanga



Diwani wa kata ya Chibe John Kisandu akizungumza wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikagua vyoo katika kata hiyo ambapo aliahidi kuhamasisha wananchi kujenga vyoo ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu



Diwani wa kata ya Chibe John Kisandu akionesha shimo la choo lililopo mbele ya familia...Shimo hilo liko wazi japokuwa limefunikwa kwa miiba,nzi wapo wa kutosha hali inayoweza kuchangia mlipuko wa ugonjwa kipindupindu



Diwani wa kata ya Chibe John Kisandu akimwagiza mama wa familia hiyo kufunika shimo la choo lililopo mbele ya familia hiyo ili kuepuka ugonjwa wa kipindupindu



Bibi hana wasiwasi....Choo changu kile paleeeeee!! 



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(kulia) akimweleza mwenyekiti wa mtaa wa Busambile bwana Charles Mayunga(mwenye kanzu) jinsi choo bora kinavyopaswa kuwa



Afisa afya wa manispaa ya Shinyanga(aliyevaa miwani) akiangalia shimo la choo kinachojengwa katika mtaa wa Busambile..ambapo alimtaka mama mwenye nyumba hiyo Severine Kulwa(katikati)kukamilisha ujenzi wa choo hicho haraka



Kushoto ni mwanasheria wa manispaa ya Shinyanga Simon Jilanga akimhoji kijana Sindi Fungwe kwanini hajajenga choo katika familia yake



Hapa ni Kata ya Kambarage-Pichani ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga akipokea maelezo kuhusu moja ya nyumba yenye wapangaji wengi ikiwa ni pamoja na ofisi ya serikali ya mtaa...Nyumba hiyo ni bora lakini hakuna choo



Muonekano wa nyumba hiyo isiyokuwa na choo bali bafu pekee kama linavyoonekana kulia likiwa na pazia la mifuko.Baada ya kusikia ugeni wa mkuu wa wilaya,mmiliki wa nyumba hiyo alitoweka


Muonekano wa mbele wa nyumba hiyo,ambapo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliagiza maduka yaliyopo katika nyumba hiyo yafungwe mpaka pale watakapojenga choo



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitafakari jambo katika mtaa wa Mwasele "A" wakati akikagua vyoo na kubaini kuwa katika mtaa huo ambao una kaya 22 zisizokuwa na vyoo na zenye vyoo vingi siyo bora


Muonekano wa choo katika familia moja mtaa wa Mwasele A kata ya Kambarage 


Kijana akipika wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga katika mtaa wa Mwasele A ..pembeni kuna choo hakijafunikwa..angalia hapa chini



Choo kikiwa wazi hali ambayo ni hatari kwa afya za watu wanaozunguka eneo hilo



Muonekano wa choo hicho kwa mbele



Hiki ni choo kingine katika mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga

Hiki choo kipo katika senta ya Maduka Matatu mtaa wa Mwasele A kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga.Ni choo cha ajabu kweli kweli..hakuna tundu isipokuwa kuna bomba na matofali mawili..ukitaka kujisaidia kwanza lazima uwe na shabaha kulenga kwenye bomba lililolazwa chini..ukikosea tu lazima uzoe hakuna ujanja...kinatumiwa na wamiliki wa maduka katika senta hiyo..angalia hapa chini


Afisa afya wa manispaa ya Shinyanga Heri Nakuzelwa akiwapa muongozo wafanyabiashara katika senta ya Maduka Matatu baada ya mkuu wa wilaya kuagiza kufunga maduka hayo mpaka wajenge choo bora kuliko kile cha kulenga..angalia hapo juu



Mfanyabiashara wa duka la dawa za binadamu senta ya Maduka Matatu akifunga duka lake



Hatuna choo..Tunafunga duka....



Wananchi wakisikiliza maelekezo kutoka afisa afya wa manispaa ya Shinyanga Heri Nakuzelwa aliyewataka wajenge vyoo ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu



Afisa afya wa manispaa ya Shinyanga Heri Nakuzelwa akitoa elimu kwa wakazi wa Mwasele wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro



Baada ya agizo la mkuu wa wilaya...maduka yakafungwa..



Baada ya Ziara..Hapa ni katika ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna akizungumza na waandishi wa habari.Kalinjuna alisema tangu ugonjwa kipindu pindu ulipuke katika manispaa hiyo wagonjwa ni 98 na waliofariki dunia ni watatu hivyo kuitaka jamii kujenga tabia ya kufanya usafi,wajenge vyoo,wafanyabiashara wa matunda kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi na vitendo vyote vinavyosababisha kuenea kwa ugonjwa huo.


Mkurugenzi huyo wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna alisema wananchi wengi hawana vyoo na wenye vyoo vingi siyo vyoo bora hivyo kuwataka kujenga vyoo bora na kuongeza kuwa tayari wamefunga maduka matano yasiyo na vyoo,kuagiza wananchi na viongozi kusimamia ujenzi wa vyoo na kwamba zoezi la kukagua,kukamata na kufunga maduka ni endelevu...Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini