Kigogo Kenya Matatani kwa Kuhudhuria Sherehe za Kuapishwa Rais MAGUFULI Dar

Gavana wa Jimbo la Siaya, nchini Kenya, Cornel Rasanga ameingia matatani akidaiwa kutumia Sh20 milioni za nchi hiyo (karibu Sh400 milioni) kutoka katika mfuko za Serikali kwa ajili safari ya kuhudhuria sherehe za kumwapisha Rais John Magufuli. 

Dk Magufuli alipishwa Novemba 5, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 25.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kenya (PAC), Nicholas Gumbo amemtuhumu Rasanga kwa kutumia fedha hizo kutoka kwenye mfuko wa Serikali wa safari.

“Gavana wa Rasanga lazima awaambie wananchi wa Siaya, imekuwaje akatumia Sh20 milioni kwenda Tanzania kwa ajili ya shughuli ya Dk Magufuli?
 
“Sidhani kama Dk Magufuli ana uhusiano wowote na wananchi wa Kaunti ya Siaya kiasi cha Gavana kutumia fedha hizo za umma kwenda Tanzania,” alisema Gumbo.

Gumbo alisema Dk Magufuli anafahamika kuwa ni rafiki mkubwa wa kiongozi wa Cord, Raila Odinga ambaye pia alihudhuria sherehe hizo.
 
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika.

Akizungumzia tuhuma hizo, Rasanga alisema madai yalitolewa na Gumbo ambaye ni Mbunge wa Rarieda, ni uzushi na alikuwa anataka kujikweza kisiasa.
 
“Hii ilikuwa safari binafsi. Hatukutumia fedha za Serikali kama inavyoelezwa,” alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation.

Gavana huyo alisema alikwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Dk Magufuli kwa mwaliko binafsi wa Rais hiyo wa Tano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema ziara yake Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
 
“Ukweli ni kwamba Rais wa Tanzania aliwahi kutembelea Siaya na tulijadiliana masuala mbalimbali ikiwamo usafiri hasa katika Ziwa Victoria,” alisema Rasanga na kuongeza:

“Dk Magufuli anatokea Kanda ya Ziwa na mpango wake mkubwa ni kuimarisha bandari katika Ziwa Victoria na kuchaguliwa kwake kuwa Rais kutarahisisha zaidi utekelezaji wa mipango yake.
 
“Hakuna sababu ya kuingiza siasa katika safari hii. Tuko katika mipango mizuri tu ya kibiashara na Tanzania ambayo kwa sasa imeanza kupanuka.”

Mwenyekiti huyo wa PAC Kenya alisema safari hiyo ya Novemba 5, ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Hata hivyo, Naibu Gavana, Wilson Ouma alipinga madai ya Gumbo akisema alikuwa na lengo la kumharibia bosi wake.
 
“Ukweli Gavana Rasanga alitumia fedha zake kwenda Tanzania na uzushi wowote unatakiwa ukomeshwe,” alisema Ouma alipozungumza na Nation.
 
Akisisitiza, Gumbo alisema ataendelea kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma unaofanywa na maofisa wa Serikali kwa kutumia vyeo vyao.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini