Ishu ya Paul Makonda kuwatupa selo watumishi wa serikali yazidi kuchambuliwa


PONGEZI HIZI KWA MAKONDA HAZIKUBALIKI!

Ndugu zangu, muda huu nimeona kwenye mitandao kadhaa watu wakifurahia hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu yetu Paul Makonda kutoa amri (ambayo imetekelezwa) ya kuwaweka ndani wataalam wa ardhi ambao walishindwa kufika eneo la kazi kwa wakati.

Binafsi siungi mkono kitendo cha watendaji kuchelewa maeneo ya kazi lakini zaidi ya yote siungi mkono kitendo cha mkuu wa wilaya kuwaweka ndani watendaji kwa kosa la kuchelewa kazini.


Madhara ya kuwachekea wakuu wa wilaya pale wanapotoa amri zinazokiuka haki za msingi za wafanyakazi ni makubwa mno. Huko nyuma tulizoea mambo haya kufanywa na wakuu wa wilaya enzi za Nyerere, hatutarajii hadi leo wakuu hawa kuendesha wilaya zao kwa amri.

Ni muhimu sana masuala ya kazi yaendeshwe kwa sheria na kanuni za kazi na huyo mtu anayefurahia mamlaka (haramu) ya ma DC kuweka watu ndani atakuwa na matatizo makubwa. Watu wanapaswa kuwekwa ndani kama wamefanya makosa kwa mujibu wa sheria na si kama apendavyo DC.

Tuijenge nchi yetu kimfumo zaidi kuliko ki-amri, nchi zinazoendeshwa kwa amri amri huwa hazifiki kokote, kama tutashindwa kujijenga kimfumo katika miaka hii mitano tukategemea kuendesha nchi kwa amri, matamko na mikwara - ikifika 2020 tutaulizana nini kilifanyika na sote tutabaki kusimulia matamko lukuki yaliyotolewa.

Nimalizie tena kwa kuwakumbusha kuwa "Afrika itajengwa na mifumo imara, watu imara hawawezi kuijenga Afrika maana siku moja watakufa, na kama watakufa bila kuacha mifumo imara - yale yote waliyoyafanya yatapotea haraka ".

Ndugu yetu DC, Paul Makonda, tujengeeni mfumo imara utakaofanya wafanyakazi wote kuwa kazini kwa wakati, (msijijenge ninyi) watu imara na amri lukuki!

SAKATA LA MAKONDA NA KUWAWEKA NDANI WATENDAJI WALIOCHELEWA – MTIZAMO WA KISHERIA;

Nilipo- post juu ya jambo hilo mjadala mkubwa wa wananchi umekuwa ni kutaka kujua sheria inaelekeza nini kwa mamlaka ya wakuu wa wilaya. Kwa uelewa wangu wa shahada ya kwanza ya sheria nimeona niwawekee hapa ufafanuzi wa kisheria kwa ajili ya faida yenu na mjadala mwingine tena.

SHERIA INASEMAJE?

Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 (The Regional Administration Act) kwenye kifungu cha 15 (1) imeweka sharti muhimu kwa Mkuu wa Wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamrisha mtu akamatwe, kifungu hicho kinamtaka afanye hivyo pale tu ambapo atakuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika athari yake huwa ni kukamatwa na kushtakiwa na tena sheria imeweka masharti ya namna ya kushtaki.

JE KISHERIA DC MAKONDA ANA HAKI YA KUWAWEKA NDANI WATAALAM HAO?

Hapana, kisheria hana mamlaka hayo, Kosa walilotenda watalaam hawa wa ardhi ni la kuchelewa kwenye eneo la kazi, kosa la kuchelewa mahali kwenye majukumu ya kawaida ya kupima ardhi haliwezi kamwe kumfanya mtu ashitakiwe hadi pale ambapo kuchelewa huko kutakuwa kumesababisha madhara makubwa na yanayoweza kuthibitishwa mahakamani. Kwa hiyo kama Makonda amewaweka ndani anawajibika kwa mujibu wa sheria hii kuwapandisha kizimbani haraka kesho (Jambo ambalo atalikwepa kwani hawana kosa ambalo lina “amount to being arrested and tried” yaani “kukamatwa na kushtakiwa”).

JE, MAKONDA AKISHTAKIWA ANAWEZA KUPEWA ADHABU GANI?

Bahati nzuri, sheria hiyohiyo katika kifungu cha 15 (1) imeeleza kuwa ikiwa mkuu wa wilaya atatumia mamlaka yaliyowekwa na kifungu husika kwa maana ya kutumia madaraka yake vibaya, atakuwa ametenda kosa na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).

Kifungu hicho cha 96 (1) na (2) kinaeleza kuwa Mtu yeyote ambaye ameajiriwa kwenye utumishi wa umma (akiwemo Mkuu wa Wilaya) anayetenda au kuamrisha utendekaji wa jambo kwa kutumia vibaya madaraka ya kazi yake, kitendo chochote cha dhuluma ambacho kinazuia haki ya mwingine atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani anaweza kufungwa miaka mitatu jela.

JE WATAALAM HAO WA ARDHI WANAWEZA KUMSHITAKI MAKONDA?

Ndiyo, wataalam wa Ardhi waliotendewa amri hiyo wanaweza kumshitaki Paul Makonda kwa kitendo chake cha kutumia vibaya madaraka yake lakini bahati mbaya itakayowakuta ni kwamba Sheria hiyo hiyo ya Kanuni ya adhabu kwenye kifungu cha 96 (3) imeweka sharti lingine kuwa Uendeshaji wa shitaka kwa husika hautaanzishwa mpaka kitakapotolewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (Kesi ya Nyani amekabidhiwa ngedere).

Nawatakia jioni njema sana.

Na. Julius Mtatiro

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini