MSHTUKO! Wazee Wanaume, Wanawake Walala Pamoja Huko Bukoba

Wazee wanaoishi katika kituo cha kulea wazee kinachomilikiwa na serikali kilichoko Kilima Bukoba Vijijini, wanalazimika kulala katika bweni moja wanaume na wanawake baada ya jengo la wazee wanawake kuezuliwa na upepo miaka minane iliyopita. 

Wakizungumzia hali hiyo wazee wanaoishi katika kituo hicho walisema kuwa tangu jengo la wazee wanawake lilipoezuliwa na upepo hadi sasa wanalazimika kukaa katika jengo moja.

Mwenyekiti wa Wazee kambini hapo, Evarister Kayogera alisema kuwa nyumba ya kulala wazee wanawake iliezuliwa muda mrefu, serikali haijairekebisha na kwamba huwa wanakuja wanaangalia tu wanaondoka hawarudi, hivyo hawafahamu lini serikali italirekebisha ili wanawake wahamie katika jengo lao ili waache kubanana sehemu moja.

Mbali na tatizo hilo mzee Kayogera alisema wamekuwa wakikosa usafiri wa kupelekwa hospitali na wakati mwingine wakipelekwa wanapimwa na kuandikiwa dawa na kuambiwa kuwa hazipo waende kununua mitaani wakati wao hawana kipato chochote. 

“Wahudumu wetu wakiwa na fedha ndiyo huwa wanachanga na kutununulia dawa, na wakati mwingine wakiwa hawana fedha wanatafuta dawa za kienyeji mbugani wanachemsha wanatupa tunakunywa ili tuone kama tutaendelea kuishi,” alisema. 
Mzee mwingine John Rwiza alisema kuwa ni muda mrefu sasa kituo hicho hakina mafuta ya taa hali inayosababisha kula na kulala gizani, kutokana na kutokuwa na umeme. 

Rwiza alisema chakula cha usiku wanalia gizani hawana mafuta ya taa na kwamba wanapika chakula mfano wali usio na mafuta wanachemsha tu na maharage hayawekwi chochote, wanakunywa uji usio na sukari na hawana pa kujisaidia.

Popular posts from this blog

Upepo wakwamisha Uokoaji Meli iliyozama

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini