ANGALIA PICHA NESI MUHIMBILI AKATWA MIGUU
Flora Nathaniel Shayo akatwa miguu baada ya kuugua kisukari.
Flora Nathaniel Shayo (60) mkazi wa Chanika, wilayani Ilala, Dar ameiomba serikali pamoja na Rais Jakaya Mrisho Kikwete imsaidie baada ya kukatwa miguu kutokana na kuugua ugonjwa wa kisukari.
Akizungumza na waandishi wetu hivi
karibuni, Flora alisema aliwahi kuwa muuguzi (nesi) katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kwa miaka 26 iliyopita na baada ya kustaafu alikuwa
akifanya biashara ya kuuza dawa za binadamu (Duka la dawa) huku mwanaye
akiwa anafanya kazi za muziki. Mama huyo aliendelea kufunguka kuwa,
aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari na presha mwaka 2006 ndipo
akaanza kutumia dawa.
CHANZO CHA UGONJWA
Akifafanua zaidi mama huyo alikuwa
na haya ya kusema: “Mwaka 2011 kidole gumba cha mguu wangu wa kulia
kilianza kukauka na kubadilika rangi nikaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Nilipofika hospitali nilipimwa na
kugundulika kuwa sumu imepanda mpaka juu karibu na goti, madaktari
wakaniambia ni lazima nikatwe mguu ili kuokoa maisha yangu. Nilipatwa na
woga, lakini sikuwa na la kufanya, nilikubali.
“Nikaandaliwa na kupelekwa katika
chumba cha upasuaji na kukatwa mguu, nilikuwa siamini kama kweli
nimekuwa kilema lakini ilinibidi niamini, kweli hujafa hujaumbika,”
alisema mama huyo huku akiwa na majonzi.
“Tangu nimekatwa mguu wa kwanza
nateseka, mwanagu Dogo Mfaume ambaye ni mwanamuziki hana uwezo wa
kunisaidia kutokana na ukweli kwamba hana kipato cha kutosha,” alisema
huku akilengwalengwa na machozi.
Flora Nathaniel Shayo kabla ya kukatwa miguu.
AKATWA MGUU WA PILI
Akasema: “Haukupita muda mrefu mguu wa pili nao ukaanza kuvimba, nilihisi kuchanganyikiwa na nikaona kuwa huo sasa ndiyo mwisho wa maisha yangu.
“Kwa kweli nilipatwa na msongo wa
mawazo na kukata tamaa ya kuendelea kuishi baada ya kwenda tena
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na madaktari kuniambia mguu wa pili nao
ukatwe, nilikatwa, namshukuru Mungu nimeuguzwa na kidonda kilipona
vizuri lakini baada ya hapo nahisi akili yangu ilihama kabisa maana
nilikuwa nahesabu siku za kuishi tu.
“Hakika mganga hajigangi. Sion
thamani ya kuishi hapa duniani, nimebaki mkiwa na kujiona nastahili
kufariki dunia maana sijui hata muelekeo wa maisha yangu utakuaje.”
OMBI KWA WATANZANIA
Baada ya kujifuta machozi kwa kanga yake aliendelea kusema: “Nawaomba Watanzania
wenzangu wanisaidie kunichangia ili niweze kupata kiti cha magurudumu
(wheelchair) kitakachoniwezesha kutoka nje na kufanya shughuli zangu.
“Ikiwezekana wanisaidie nipate
miguu ya bandia, maana nashindwa hata kwenda nyumba ya ibada kusali au
kufanya shughuli ndogondogo wakati bado nina nguvu kabisa ya kujitafutia
riziki na kujenga taifa langu.”
OMBI KWA RAIS
Alimgusa Rais Kikwete huku
akitiririka machozi akasema: “Namuomba Rais Kikwete aniangalie kwa kuwa
nilifanya kazi Muhimbili kwa muda mrefu na pesa niliyoipata baada ya
kustaafu haikuweza kukimu mahitaji yangu mpaka sasa nimebaki kama yatima
tu.
Akikabidhiwa cheti baada ya kuhitimu kozi ya unesi.
“Watoto wangu hawana uwezo na msaada nilioupata hospitali ni wa matibabu tu pale nilipohitajika
kukatwa mguu, nahitaji dawa za kila siku, chakula na mahitaji mengine
na dawa za kisukari ni gharama sana, kuna wakati nakosa hata pesa ya
kununulia kwani presha pia inanisumbua.”
ATOA NENO KWA WASANII
“Kwa kuwa mwanangu Dogo Mfaume ni
msanii, nawaomba rafiki zake na wasanii wenzake wanisaidie kwani hali
niliyonayo ni mbaya, mpaka sasa naishi tu kwa matumaini. Kuna siku nakosa hata hela ya kwenda kujitibu,” alisema mama huyo kwa uchungu.
Naye Dogo alipotafutwa kuzungumzia
ishu hiyo alisema, kwa sasa mambo yake hayapo sawa ndiyo sababu
anashindwa kukidhi mahitaji ya mzazi wake.
“Kusema kweli hali ya mama
inaniumiza sana kichwa, nashindwa hata kuelewa cha kufanya, nashindwa
kumudu mahitaji yake ipasavyo ni tatizo kikubwa
ningependa kwa yeyote ambaye yupo tayari kumsaidia basi asisite, siku
zote mimi namuombea kwa Mungu mzazi wangu,”alisema Dogo Mfaume.
Yeyote aliyeguswa na habari hii na
angependa kumsaidia awasiliane na mama huyu kwa namba 0755 216 865,
kutoa ni moyo, sioyo utajiri.