MASIKINI MGUNDUZI WA TANZANITE MZEE NGOMA ANAZIDI KUTESEKA PAMOJA NA KUGUNDUA MADINI YENYE THAMANI KUBWA KWA TAIFA!!
Jumanne Ngoma: Mgunduzi wa tanzanite anayetaabika
- Pia amegundua madini ya jasi yanayotengeneza saruji
- Apigania kupata sehemu ya mauzo yake bila mafanikio
- Mkubwa serikalini alimpora sarafi yake Soko la Dunia
- Ahoji iweje Williamson alipwe kwa kugundua almasi?
Tanzanite ni madini ghali duniani yanayozalishwa nchini Tanzania pekee. Mwandishi Wetu MAYAGE S. MAYAGE amefanya mahojiano na mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Ngoma kijijini kwake Makanya, Same, Kilimanjaro. Katika sehemu hii ya kwanza ya makala, pamoja na mambo mengine, Ngoma anaeleza jinsi alivyodhulumiwa haki yake na jitihada anazoendelea kufanya ili walau familia yake ifaidike na sehemu ya mauzo ya madini hayo.
“MAONI yangu ni kuwa utundu na uvumbuzi popote duniani, hulipwa na unatiliwa thamani sana katika nchi za kikabaila na kijamaa. Pendekezo langu, alipwe haki zake zote anazostahili.”
Hilo ni dokezo la aliyekuwa Msaidizi wa Rais (Uchumi), Profesa Simon Mbilinyi, katika jalada lililokuwa na barua ya Jumanne Mhero Ngoma, ambayo alikuwa akiiomba Serikali imlipe haki yake ya kuwa mgunduzi wa madini ya tanzanite ambayo yametokea kuwa na thamani kubwa sana katika soko la dunia.
Ngoma, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 68, ndiye mgunduzi wa madini hayo ambayo kama Serikali ingekuwa makini tangu ayagundue mwaka 1967, yangekuwa yameiweka nchi hii katika ramani nyingine kabisa ya kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na dokezo hilo la Ikulu, la Oktoba 8, 1980, tena kutoka kwa Mshauri wa Rais katika Masuala ya Uchumi, Ngoma aliambulia hundi ya Sh 352,448.25 tu kutoka serikalini, ambayo ililipwa kutokana na ushauri huo.
Kana kwamba Serikali inatambua, na wala haina shaka juu ya ugunduzi wake huo, iliendelea kumuenzi Ngoma kwa kazi yake nzuri hiyo, kwa kuwa miongoni mwa watu waliotunukiwa tuzo ya ngao na cheti, pamoja na fedha taslimu Sh 50,000 katika sherehe za Mei Mosi, zilizofanyika kitaifa mkoani Mbeya mwaka 1984.
Kwa mujibu wa Ngoma, heshima hiyo aliyopewa na Serikali ilikuwa inaambatana na safari ya nje, ya kwenda kutembelea soko la dunia la tanzanite pamoja na kuzuru viwanda maarufu duniani vinavyotengeneza bidhaa zinazotokana na madini hayo ya tanzanite.
Hata hivyo, katika hali ya masikitiko makubwa, Ngoma anasema safari hiyo hakuwahi kuipata, na badala yake mjanja mmoja mkubwa tu katika Serikali hiyo ya Awamu ya Kwanza, tena anayemtaja kwa jina, ingawa kwa sasa ni marehemu, aliipora safari yake hiyo kimya kimya, na akampeleka mtoto wake wa kiume, ambaye bila aibu alisafiri kwa jina halisi la Jumanne Ngoma, kama mgunduzi wa tanzanite.
Ngoma aliugundua vipi ujanja wa mtu huyo? Anasimulia: “Baada ya kukabidhiwa ngao, cheti na kiasi hicho cha fedha (Sh 50,000) na Mzee Rashid Kawawa kule Mbeya, aliniambia nikishafika nyumbani nijiandae, Serikali ilikuwa imeniandalia safari (tour) ya kwenda kutembelea nchi mbalimbali zinazosifika kwa kuwa na migodi ya madini huko Ulaya, soko la dunia la tanzanite na viwanda vinavyotengeneza bidhaa zitokanazo na tanzanite.
“Nilifika nyumbani kwangu hapa Makanya (Same, Kilimanjaro), nikajiandaa nikisubiri barua ya kuitwa Dar es Salaam tayari kwa safari. “Siku moja nikiwa shambani, alikuja mtu mmoja akaacha barua hapa. Nilipotoka shamba watoto wakaniambia; baba kuna barua yako hapa…nikajua, safari yangu imeiva. Niliingia ndani nikatulia, na kisha nikaifungua. Humo nikakuta boarding ticket (kipande kinachomruhusu abiria kuingia ndani ya ndege) zilizokwishatumika, kadi ya chanjo ya homa ya manjano na vikorokoro vingine vinavyoelezea nchi na mahali mtu huyo alikotembelea, vyote vikiwa na jina langu.”
Kwa hakika, ukimsikiliza Ngoma katika masimulizi yake juu ya vitimbi alivyofanyiwa na mamlaka zinazohusika na madini pamoja na Serikali kwa ujumla, kama ni mtu unayeguswa, unaweza ukatokwa machozi.
Katika muda wote wa mazungumzo haya yaliyofanyika nyumbani kwake, kijijini Makanya, Same, mkoani Kilimanjaro, Ngoma alikuwa ni mtu wa kulaani, kulalamika na kujiapiza.
Na hafichi kuonyesha ghadhabu yake kwa michezo yote michafu anayofanyiwa na wasiomtakia mema.
Anasema kwa mfano: “Kwa bahati nzuri sana, wote walionifanyia vitimbi na kunizibia riziki yangu, wamekufa vifo vibaya. Wengi wao hawapo duniani. Mungu ananilipa, anawaadhibu na naamini ataendelea kuwaadhibu wote wanaokalia haki yangu.”
Hata baada ya kupata taarifa ya kufikiwa na Rai, ili pamoja na mambo mengine azungumzie ugunduzi wake huo, Ngoma hakuwa na hamu ya kufanya hivyo, akisema haoni faida yoyote ya yeye kuendelea kuzungumza na vyombo vya habari juu ya ugunduzi wake huo, kwa maelezo kwamba hafaidiki chochote, si tu kutoka kwenye vyombo vyenyewe vya habari, bali hata serikalini.
Kwa mfano, katika moja ya karatasi alizokuwa ameandika maelezo yake kwa mkono wake tayari kwa mahojiano haya, Ngoma anaandika:
“Karibu sana kijijini kwetu hapa Makanya, jisikie uko nyumbani. Mimi ndiye Jumanne Mhero Ngoma mgunduzi wa madini ya tanzanite. Nimehojiwa mara nyingi sana na magazeti mbalimbali nchini pamoja na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), lakini sijaona faida ya mahojiano hayo.
“Nimehojiwa na waandishi wa habari wa BBC (Shirika la Utangazaji la Uingereza) mwaka jana, nikiwa Arusha, ambao ni Abdallah Majura na Tido Mhando, na mahojiano hayo yakarushwa hewani na BBC, London. Nawe leo unanifuata. Je, ni kwa faida ya kuuza magazeti yenu tu au na mimi nitafaidikaje juu ya mahojiano haya?”
Kwa ufupi, Ngoma alitaka kwanza ahakikishiwe ni kifuta jasho kiasi gani ambacho angelipwa kwa mahojiano haya. Na kwa kuwa mwandishi hakuwa amejiandaa kwa hilo, na kutokana na ukweli kwamba swali lenyewe hilo la malipo lilikuwa ni la kiutawala, ilibidi ifanyike juhudi kidogo kumshawishi ili kufanikisha mahojiano haya.
Kwa wanaokifahamu kijiji cha Makanya, wanatambua kwamba moja ya sifa za kijiji hicho ni kuwa na madini mengi ya jasi (gypsum), ambayo ni muhimu sana katika viwanda vya saruji nchini kwa uzalishaji wa saruji. Aidha, madini hayo hutumika katika utengenezaji wa chaki na POP zinazotumika hospitalini.
Mgunduzi wa madini hayo ya jasi kijijini hapo si mwingine, bali ni Ngoma. Huyo ndiye alikuwa msambazaji (supplier) wa kwanza wa madini hayo wakati Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill kilipoanza uzalishaji wa bidhaa hiyo miaka ya katikati ya sitini.
Kutokana na ugunduzi wake huo wa jasi, madini ambayo ndiyo tegemeo la kiuchumi kwa wakazi na pato la Kijiji cha Makanya, uongozi wa kijiji hicho, katika kumuenzi Ngoma, umemsamehe kushiriki katika shughuli yoyote ya uchangiaji wa miradi ya maendeleo kama vile shule, zahanati na/au miradi ya maji.
Anasema: “Nashukuru sana, uongozi wa kijiji na wanakijiji wenzangu wanatambua mchango wangu katika maendeleo ya hapa. Katika kuenzi ugunduzi wangu wa madini ya jasi, wamenisamehe nisishiriki aina yoyote ya ‘msaragambo’ (harambee ya kuchangia maendeleo).”
Hata hivyo, pamoja na Ngoma kuenziwa na wanakijiji wenzake kuhusu ugunduzi wake huo wa madini ya jasi, madini ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia katika kukua kwa uchumi wa wanakijiji cha Makanya, ana malalamiko mengi kwa watawala wa nchi hii kwa kutotaka afaidike na ugunduzi wake madini ya tanzanite.
Anasema juhudi zake zote za kutaka Serikali imsaidie kumpatia Hati ya Ulindaji wa Kazi za Kigunduzi (Intellectual Property Protective – IPP), ambayo ingemsaidia kutambuliwa kimataifa na hivyo kufaidika na ugunduzi wake huo kama ambavyo mgunduzi wa almasi ya Mwadui, Williamson anavyofaidika, zimegonga mwamba.
Katika kilio hicho, anasema: “Kama familia ya Williamson, mgunduzi wa almasi Mwadui, inavyofaidika na ugunduzi huo, nami naomba Serikali isimamie kwa kuwapo maandishi yanayosema kwamba nitakuwa napata asilimia fulani ya mapato yanayotokana na mauzo yote ya tanzanite kwa maisha yangu yote na kizazi changu hadi madini hayo yatakapokwisha.
“Msajili wa Kulinda Haki za Ugunduzi, aliniandikia barua akisema ugunduzi tu wa madini katika ardhi, hauwezi kupewa Hati ya Kulinda Kazi za Ugunduzi. Sawa; lakini mbona Williamson yeye alipewa? Yeye aligundua almasi ya Mwadui angani, kwenye mwezi au baharini? Si ni katika ardhi hii hii ya Tanzania, ambamo nami nimegundua tanzanite?”
Ni katika mkanganyiko huo, Ngoma alitumia fursa hii kuiomba rasmi Kamati ya Madini ya Rais, chini ya Jaji Mark Bomani, kabla ya kuhitimisha kazi yake hiyo, imwite mbele ya kamati hiyo ili aweze kuwasilisha maoni yake juu ya nini kifanyike katika sekta ya madini.
Lakini pia, Ngoma haachi kulaani baadhi ya kauli za viongozi waandamizi serikalini ambao wamekuwa wakimwekea ‘ukuta’ kila anapofuatilia haki zake, wakisema ni mtu asiyetosheka hata akipewa fedha inayolingana na Mlima Kilimanjaro.
“Hivi Sh 352,448.25, nilizopewa na Serikali ndizo ninazosimangiwa kwamba sitosheki hata nikipewa fedha zinazolingana na Mlima Kilimanjaro? Kama ni kutosheka, kwa nini viongozi hao hao wao hawataki kutosheka na madaraka yao?
“Mbona wamestaafu, lakini juzi tumewaona wakichukua fomu za kuomba uongozi wa juu katika chama?” anahoji Ngoma bila kutaja jina la kiongozi wa ngazi ya juu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, ambaye alipata kumwambia kwa ukali kwamba hatosheki hata akipewa fedha zinazolingana na Mlima Kilimanjaro.
Ngoma aliyagundua vipi madini ya zoisite, ambayo baadaye yalikuja kubadilishwa jina na kuitwa tanzanite kutokana na ushauri wa kampuni moja ya Kimarekani, iliyokuwa ikifanyia biashara yake mjini Arusha, ikijulikana kwa jina la Tiffany kwa Serikali?
Je; unayajua maisha anayoishi mgunduzi huyo wa tanzanite, na ndoto zake alizonazo katika umri wake wa sasa, juu ya ugunduzi mwingine wa madini, yakiwamo hayo ya tanzanite?
Unafahamu kama Ngoma ana kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya kampuni ya kigeni ya AFGEM, kwa sasa Tanzanite One, akitaka kampuni hiyo imlipe fidia ya Sh bilioni mbili taslimu kwa madai kwamba kampuni hiyo, kwa makusudi tu, imepotosha katika jarida lao linalochapishwa nchini Afrika Kusini, kwa kuandika kwamba mgunduzi wa tanzanite ni mtu mmoja anayetajwa kwa jina la Ali juu ya watu, na si yeye Jumanne Ngoma? Soma yote hayo katika toleo letu lijalo la Rai.
Chanzo: Gazeti la RAI