UKATILI: INASIKITISHA SANA...MTOTO ABAKWA NA KUUAWA KINYAMA HUKO SHINYANGA!
Mazishi
ya mwanafunzi aliyeuawa kikatili kwa kubakwa kisha kutobolewa macho na
watu wasiofahamika kisha mwili wake kutupwa kichakani katika kijiji cha
Nhelegani kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga yamefanyika
katika makaburi ya familia katika kijiji cha Negezi kata ya Mwawaza
katika manispaa ya Shinyanga.
Mwanafunzi
huyo aliyekuwa anasoma darasa la tatu katika shule ya Msingi Negezi
iliyopo kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga alikutwa ameuawa kwa
kubakwa kisha kutobolewa Agosti 25 mwaka huu saa saba mchana katika
kitongoji cha Kashampa kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi.
Akizungumza
wakati wa mazishi ya mwili wa marehemu yaliyofanyika LEO MCHANA naibu
meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila alilaani kitendo cha kinyama
alichofanyiwa mtoto huyo huku akiitaka jamii kushirikiana na jeshi la
polisi katika kuwafichua wahusika wa mauaji hayo.
“Kifo cha
mtoto huyu ni mapenzi ya mungu yaliyosababishwa na wanadamu
wabaya,naomba suala la hili lifuatiliwe hatuhitaji siasa katika hili
inauma sana kwani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinatishia amani
Shinyanga”,alieleza Nkulila.
Kwa
upande wake Intelijensia mkoa wa Shinyanga Bundala Maige alisema suala
la ulinzi kwa watoto ni jamii nzima na kwamba wahalifu wako ndani ya
jamii hivyo kuitaka jamii kuwafichua wahalifu hao ili kukomesha vitendo
vya ukatili vinavyoendelea mkoani Shinyanga.
Naye
mwenyekiti wa mtaa wa Masekelo kata ya Masekelo yalikofanyika mazishi ya
mtoto huyo bwana Peter Juma Kitundu alisema kifo cha mtoto huyo kinatia
simanzi kubwa kwani kimesababishwa na binadamu huku akiiomba serikali
kulifanyia uchunguzi wa kina tukio hilo na lisiingizwe suala la siasa.
Kwa
upande wake mwinjilisti Emmanuel Donald Kaswalala aliyeendesha ibada ya
mazishi alilaani vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watotot huku
akiiomba jamii kumrudia mwenyezi mungu kwa kuondokana na matendo mabaya.