DAKTARI ABAMBWA NA MAITI DUKANI


Bw.Prosper Samson anayedaiwa kuwa ni daktari feki, akiwa nyumbani kwake.
UKANJANJA! Jeshi la Polisi wilayani Ikungi, Singida linamshikilia daktari anayedaiwa kuwa ni feki, Prosper Samson (pichani) kwa madai ya kumtibu mgonjwa Jibuli Mahende, mkazi  Kijiji cha Iyumbu, Sepuka na kumsababishia kifo chake, Uwazi linakupa mkasa huo kwa kina.
Habari zinadai kuwa, Jibuli alifariki dunia hivi karibuni baada ya kutibiwa na mtu huyo anayejiita daktari kutokana na kile kilichodaiwa kuwa alizidishiwa dozi kwa kuongezewa chupa tisa za maji ya drip sanjari na vidonge sita ambavyo havikujulikana jina mara moja.
HISTORIA YA MAREHEMU
Kwa mujibu wa ndugu, marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua, kiuno na mgongo ambapo daktari huyo alimpa dawa hizo muda mfupi baadaye Jibuli alipoteza maisha akiwa kwenye duka la dawa, nyumbani kwa Prosper.
Bw.Prosper Samson akiwa chini ya ulinzi katika duka lake la dawa.
MGANGA MKUU WA WILAYA ASIMULIA
Akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa Wilaya ya Ikungi, mmoja wa madaktari wa wilaya hiyo, Philip Kitundu alisema tukio hilo lilitokea juzikati saa nne asubuhi kwenye vyumba maalum vilivyotengwa na daktari huyo kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali za matibabu.
“Baada ya kupewa taarifa za kifo hicho na utete wake, kesho yake tulikwenda kukagua duka la dawa la mtu huyo,” alisema daktari huyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo, walipofika dukani kwa Prosper anayejitangaza kuwa ni daktari wa magonjwa ya binadamu, walilikagua na kugundua kuwa hakuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) inayomruhusu kufanya biashara hiyo na alikiri kuwa hakuwa na cheti  cha chuo chochote alichosomea udaktari.
Marehemu Jibuli Mahende, aliyepoteza maisha chini ya mikono ya daktari feki. 
“Hata tulipopekuwa dukani kwake tulikuta dawa ambazo haziruhusiwi kabisa kwenye maduka ya dawa muhimu, tulikuta dawa na sindano na dawa za vidonda. Alikuwa anawafunga vidonda watu, analaza na anatoa huduma za kujifungua kwa akina mama,” alifafanua daktari huyo.
YADAIWA NI MTU WA TATU KUFA
Daktari huyo wa wilaya aliongeza kusema kwamba katika ukaguzi huo walikuta pia dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi na kuwa tukio la Jibuli kupoteza maisha ni la tatu kwa watu waliopatiwa matibabu katika duka hilo, wawili walifia nje ya duka.
MTUHUMIWA ATOA MAELEZO
Kwa upande wake daktari huyo anayedaiwa ni feki, licha ya kukiri kumpokea mgonjwa huyo akiwa na hali mbaya na kwamba baada ya kuchukua historia yake aligundua alikuwa akisumbuliwa na kifua na kabla ya kupelekwa kwake alianza matibabu kwa waganga wa tiba asilia.
“Walikuja kwangu ili wapate ushauri lakini jinsi nilivyomwona mgonjwa nikawashauri wafanye mikakati apelekwe sehemu nyingine kwani niligundua ana matatizo tangu Juni, mwaka jana,” alisema Prosper.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Godfrey Kamwela akifafanua jambo.
MTOTO WA MAREHEMU NAYE ANENA
Naye mtoto wa marehemu Jibuli aitwaye Jilala alisema siku ya tukio asubuhi alikwenda kumsalimia baba yake na kumkuta akiwa hoi, ndipo alipoamua kumpeleka kwenye duka hilo la dawa ambapo baada ya uchunguzi wa ‘daktari’ huyo aliambiwa baba yake alisumbuliwa na kifua, mgongo na kiuno.
“Baada ya dokta kunifahamisha ugonjwa unaomsumbua baba, niliondoka kurudi nyumbani kutafuta fedha za kumuondoa pale dukani ili  kumpeleka Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi,” alifafanua mtoto huyo.
Akaendelea: “Hata hivyo, kabla ya baba hajapoteza maisha alipokuwa dukani kwa dokta alipewa vidonge sita vya dawa ambazo sikufahamu zinatibu ugonjwa gani na ilipofika saa nne asubuhi alifariki dunia, nikamsusia na kuita watu kuja kuiona maiti ya baba.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Godfrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Popular posts from this blog

Kocha mpya wa muda wa Chelsea kabidi awaambie ukweli mashabiki wa Chelsea, hii ndio kauli yake …

Walimu wadaiwa kuacha vipindi kukimbilia kufanya kazi migodini